Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
BUNGE limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria ya tasnia ya sukari, kwamba wasambazaji wa bidhaa hiyo ni miongoni mwa watu watakaotakiwa kusajiliwa pamoja na kupewa leseni.
Akiwasilisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali ya mwaka 2020, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi, alisema marekebisho hayo yana lengo la kuhakikisha kuwa Bodi ya Sukari inasimamia watu wote wanaofanya shughuli zinazohusiana na sukari.
Alisema kifungu kipya cha 11b kinapendekezwa kuongezwa ili kuweka masharti ya usajili wa wazalishaji wa sukari, ambacho ni moja kati ya vigezo vya kupata leseni ya kuzalisha bidhaa hiyo.
Profesa Kilangi alisema kifungu cha 14 cha sheria hiyo kinarekebishwa ili kuwapa wazalishaji jukumu la uingizaji sukari kwa matumizi ya kawaida, lengo ni kuongeza uwazi katika uingizaji kwa matumizi ya kawaida.
“Kifungu cha nne kinarekebishwa ili kujumuisha wasambazaji wa sukari miongoni mwa watu wanaotakiwa kusajiliwa ama kupewa leseni na Bodi chini ya sheria hiyo.
“Marekebisho haya yana lengo la kuhakikisha kuwa Bodi inasimamia watu wote wanaofanya shughuli zinazohusiana na sukari,” alisema Profesa Kilangi.
Alisema kifungu cha tisa cha sheria hiyo nacho kinarekebishwa ili kuhakikisha kuwa majukumu mahsusi ya mamlaka nyingine yanatekelezwa na mamlaka husika.
Profesa Kilangi alisema kwa sasa kifungu hicho kinampa mkurugenzi mamlaka ya kuidhinisha uingizaji mbegu za miwa nchini wakati TOSCI ndiyo chombo mahsusi chenye mamlaka ya kudhibiti masuala yote yanayohusu mbegu nchini.
Alisema kifungu cha 11A kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kupanua wigo wa ushiriki wa wadau katika kupanga bei elekezi za miwa.
“Marekebisho yanayopendekezwa yanalenga kuhakikisha kuwa wakulima na wazalishaji wa miwa wanashiriki ipasavyo katika mchakato wa kubaini gharama ya uzalishaji ambayo itakuwa kigezo cha kufikia bei elekezi,” alisema Profesa Kilangi.
Alisema kifungu cha 16 kinafutwa na kuandikwa upya kwa lengo la kukiboresha na kubainisha adhabu kwa makosa ya kuingiza na kutoa sukari nchini bila ya kuwa na leseni iliyotolewa kwa mujibu wa sheria.
Profesa Kilangi alisema kifungu kipya cha 34b kinaongezwa kwa lengo la kuweka masharti ya ufungashaji wa sukari kufanywa na wazalishaji peke yao.
Alisema kifungu hicho kinazuia ufungashaji wa sukari kwa lengo la kubadili jina halisi.
Sheria zingine zilizopitishwa na kufanyiwa marekebisho ni Sheria ya Mawakili (Sura ya 341), Sheria ya Mfuko wa Pembejeo (Sura ya 401), Sheria ya Umeme (Sura ya 131), Sheria ya Mbolea (Sura ya 378), Sheria ya Misitu (Sura ya 323), Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Mifugo (Sura ya 180).
Zingine ni Sheria ya Tafsiri ya Sheria (Sura ya 1), Sheria ya Taasisi za Kazi (Sura ya 300), Sheria ya Ulinzi wa Taifa (Sura ya 192), Sheria ya Hifadhi za Taifa (Sura ya 282), Sheria ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (Sura ya 284), Sheria ya Mbegu (Sura ya 308) na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Sura ya 283).