30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wajue ‘Madogo’ wanaopita njia za baba zao

WAHENGA walisema ‘mtoto wa nyoka ni nyota’. Usemi huu ni maarufu katika jamii, ukiwa na maana kwamba, mara nyingi watoto urithi vipaji au matendo ya wazazi wao, yawe mazuri au mabaya.

Katika dunia ya soka usemi huu pia unaendelea kuchukua nafasi yake.

Wapo wanasoka waliowahi na wanaoendelea kutamba duniani kwa sasa, lakini pia nyayo zao zikionekana kufuatiliwa na watoto.

Makaya haya yanakuletea orodha ya watoto wa mastaa waliowika na wanaoendelea kuwika katika soka, wanaofuata mkondo ule ule wa baba zao.

Watoto ninaowaorodhesha hapa, tayari wameingia katika mikataba ya soka la kulipwa, baada ya kubainika wana vipaji vya hali ya juu, kama ilivyo kwa wazazi wao.

Daniel Maldini 

Ni mtoto wa gwiji wa zamani wa klabu ya AC Milan na timu ya taifa ya Italia, Paulo Maldin.

Paulo alicheza mechi 902, zikiwemo 647 za Ligi Kuu ya Italia, Seria A na kushinda mataji matano ya Ulaya na saba ya Ligi Kuu na Kombe la Dunia mara moja. Lakini kwa ujumla alishinda mataji 23 ya mashindano mbali mbali.

Mwanae Daniel mwenye umri wa miaka 17, ameonekana kufuata nyayo za baba, ambapo tayari amejiunga na AC Milan.

Daniel alianza kuichezea Milan wiki iliyopita katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Bayern Munich.

Kuna  uwezekano AC Milan ikamkabidhi Daniel jezi namba tatu ambayo ilisitishwa matumizi, baada ya baba yake Paulo kustaafu.

Justin Kluivert

Justin mwenye umri wa miaka19, ni mtoto wa staa wa zamani wa timu za Ajax ya Uholanzi, AC Milan na Barcelona, Patrick Kluivert.

Kluivert pia  alipata kuichezea timu ya taifa ya Uholanzi, akifunga mabao 40 na kuisaidia kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1998.

 Katika kipindi chote cha uchezaji soka la kulipwa, Kluivert alifanikiwa kufunga mabao 205. 


Alishinda mataji kadhaa , ikiwemo lile la Eredivise mara mbili, La Liga na Ligi ya Mabingwa, ambapo alifunga bao la ushindi wakati alipokuwa na umri wa miaka 18.

Justin nae ameonekana kufuata nyayo zile zile za baba yake, kwani baada ya kuonesha kiwango kizuri Ajax mwaka 2018 alisainiwa na Klabu ya AS Roma.

Anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika kikosi cha kwanza cha AS Roma, kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa msimu uliopita,  baada ya kufunga dhidi ya Viktoria Plzen.

Hilo pia lilikuwa bao lake la kwanza la klabu hiyo.

Wengine walitarajia angerithi jezi ya baba yake, lakini ameamua kuvaa jezi namba 34 ili kumuenzi rafiki na mchezaji mwenzake baba yake, Abdelhak Nouri ambaye alipatwa na mshtuko wa moyo mwaka 2017 na hivyo kustaafu soka.

Timothy Weah

Ni mtoto wa staa wa zamani wa  AC Milan na timu ya Taifa  ya Liberia, George Weah. Weah kwa sasa ni Rais wa Liberia.

Juni mwaka huu, Timothy mwenye umri wa miaka 19, alitia saini mkataba wa miaka mitano wa kuichezea Klabu ya Lille, baada ya dili lake ya kujiunga na PSG ambako kuna mastaa kama Neymar, Edinson Cavan na wengine kushindikana. Alianzia soka katika klabu ya New York Red Bull ya nchini Marekani.

Baba yake, ni Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya Ballon d’Or na hakuna mwingine mpaka sasa. 

George alianza kupata umaarufu nchini Ufaransa akiwa na Monaco kabla ya kusajiliwa na kocha  Arsene Wenger wa dau la pauni 12,000.

Akiwa na AC Milan, alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu.

Anakumbukwa zaidi baada ya kuambaa na mpira na kuwalamba chenga karibia wachezaji wote wa klabu ya Hellas Verona kabla ya kufunga. George katika maisha yake ya kucheza soka la kulipwa alifunga mabao 200.


Ianis Hagi

Ni mtoto wa staa wa zamani wa klabu za Real Madrid, Barcelona,Galatasaray na timu ya Taifa ya Uturuk, Gheorghe Hagi aliyetamba miaka ya 80 hadi tisini .

Tayari chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20, amethibitisha kuwa ni kipaji kingine tishio katika soka, kwani Julai mwaka huu, aliifungia Uturuk  mabao mawili dhidi ya Romania, katika mashindano yaliyoshirikisha wachezaji wenye  umri chini ya miaka 21.

Akiwa na Genk, amechaguliwa mara mbili kama mchezaji bora wa mchezo.


Alianzia soka klabu ya Viitorul ya Uturuk kabla ya kutua Genk  ambayo imewatoa wakali kama Kevin De Bryune, Divock Origi na Thibaut Courtois.


Luca Zidane

Ni mtoto wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Juventus na timu ya Taifa ya Ufaransa, Zinedine Zidane. Zinedine kwa sasa ni kocha wa Real Madrid.

Zinedine ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi waliopata kutokea duniani, akiwa ameshinda kila kitu ambacho mchezaji na kocha angetamani kushinda.

Mwanae Luca mwenye umri wa miaka 21, naye ameonekana kufuata nyayo zile zile za baba yake, tofauti yao ni kwamba yeye ni kipa wakati baba yake alikuwa kiungo mshambuliaji.

Luca amekuzwa katika akademi ya  Real Madrid, kabla ya kuchezea timu ya wachezaji wa ziada na kisha kupandishwa kikosi cha kwanza.

Hata hivyo kwa sasa anaichezea kwa mkopo Racing Santander akitokea Real Madrid. Pia amezichezea timu za umri tofauti za vijana za Ufaransa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles