NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM
MWANASIASA na mwanasheria mkongwe nchini, Dk. Masumbuko Lamwai, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Dk. Lamwai ambaye pia ni mmoja wa waanzilishi wa Chama cha NCCR Mageuzi, wakati wa uhai wake aliweka rekodi ya kuwa diwani na mbunge wa kwanza wa upinzani Dar es Salaam kupitia chama hicho.
Akizungumza jana, mdogo wake ambaye pia ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alisema kaka yake alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.
Alisema baada ya kuzidiwa alipelekwa Hospitali ya Rabininsia Memorial iliyopo Tegeta, Dar es Salaam, lakini baada ya kupimwa madaktari walisema alikwishafariki dunia.
“Afya yake ilidhoofu katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, alipigwa na malaria kali, alikuwa anaendelea kupata dawa, hata Jumapili alikaa na watoto wake wakaongea sana, ni kwa vile tu mtu huwezi kujua kwamba Mungu amepanga aondoke saa ngapi.
“Jana (juzi) usiku ndiyo akazidiwa na katika safari za kumpeleka hospitali akafia njiani saa 9:45 alfajiri,” alisema Selasini.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo na kwamba wanaendelea na mipango ya mazishi.
Kwa mujibu wa Selasini, Dk. Lamwai pia ana kampuni ya uwakili (Lamwai advocates) na watoto wake wanne ambao ni mawakili wanafanya kazi katika ofisi hiyo.
“Dk. Lamwai ametuongoza kwa hekima na busara hadi mwisho wa uhai wake, alitengeneza msingi mzuri ambao umetusaidia sisi wengine katika familia.
“Kwa kweli tumepata pengo kubwa katika familia, tulipotelewa na wazazi, yeye alibaki kuwa kiongozi wetu na sasa ameondoka, ni pengo halizibiki, ingawa maisha yataendelea, lakini tuko na masikitiko, ni msiba mkubwa.
“Ni mtu hodari, alikuwa na msimamo, akikusudia jambo lake anapambana nalo mpaka ahakikishe limefika mwisho, mara nyingi alipenda kushirikiana na watu kufanya jambo. Hata sisi wadogo zake si kwamba alikuwa akiagiza halafu anasubiri mrejesho, akiagiza mnakwenda kufanya pamoja,” alisema Selasini.
Alisema pia baada ya kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alijiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini Kampasi ya Dar es Salaam akiwa mkuu wa kitivo cha sheria chuoni hapo.
“Alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa miaka mingi, wako mahakimu, majaji, mawakili wengi waliopita mikononi mwake… familia yetu ina wanasiasa na walimu wengi, kwa hiyo alipenda sana kazi ya ualimu,” alisema Selasini.
SIASA
Mwaka 1994 Dk. Lamwai aligombea udiwani katika Kata ya Manzese kupitia NCCR Mageuzi na katika uchaguzi mkuu wa 1995, alijitosa tena kugombea ubunge katika Jimbo la Ubungo na kushinda.
Wakati akiwa diwani, pia aliwahi kugombea umeya wa Dar es Salaam, lakini aliambulia kura moja tu.
Aidha baada ya kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Benjamin Mkapa alimteua kuwa mbunge.
KESI ZA UCHAGUZI
Dk. Lamwai atakumbukwa kwa mchango wake kwani alihusika katika kesi nyingi hasa zile za kupinga matokeo ya uchaguzi.
Miongoni mwa kesi zilizompatia umaarufu mkubwa ni ile ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Jimbo la Temeke, Ramadhani Kihiyo (1995).
NCCR Mageuzi ilikwenda mahakamani kupinga kwa madai kuwa Kihiyo alitumia vyeti visivyo vyake.
Hata hivyo kabla ya hukumu Kihiyo alijiuzulu kwa madai ya afya.
Kesi nyingine ni ile ya kupinga ushindi wa Onesmo Nangole aliyekuwa mbunge wa Longido (2015) ambapo Dk. Lamwai alikuwa akimtetea Dk. Steven Kiruswa.
Dk. Kiruswa alikwenda mahakamani kupinga ushindi na kufanikiwa hatimaye kukafanyika uchaguzi mdogo ambao alishinda kwa kupata
kura 41,258 sawa na asilimia 99.1.
Aidha mwaka 2005 Dk. Lamwai na hayati Dk. Sengondo Mvungi walichaguliwa kuvitetea baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo vilifungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi, hata hivyo baadaye kesi hiyo ilikufa.