Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kamati aliyounda kuchunguza ajali ya lori la mafuta iliyotokea Agosti 10, mwaka huu mkoani Morogoro, imekamilisha majukumu yake.
Akizungumza wakati akitoa hoja ya kuahirisha bunge, bungeni jijini Dodoma leo Ijumaa Septemba 13, amesema baada ya tukio hilo la kusikitisha, Agosti 12 aliunda Kamati Maalumu kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
“Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali, mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo kabla na baada ya ajali kutokea.
“Tayari kamati hiyo imekamilisha majukumu yake na mamlaka husika zimeelekezwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa wale wote ambao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo,” amesema.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro baada ya lori la mafuta kupinduka na kulipuka na kusababisha vifo vya watu 104 na watu zaidi ya 70 kujeruhiwa.