28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Waliokutwa na meno ya tembo wabanwa

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WATUHUMIWA sita waliokamatwa na kontena la meno ya tembo yenye thamani zaidi ya Sh bilioni saba visiwani Zanzibar, wamesomewa mashtaka matatu mapya ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa walisomewa mashtaka hayo jana na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi, mbele ya Hakimu Mkazi, Shahidi Huruma.
Nchimbi aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Mohammed Mussa (45), Mohammed Hajji Udole (42), Juma Makoma (43), Mohamed Hija au Mashaka, Omary Ally na Haider Ahmed, wote kutoka Zanzibar.
Washtakiwa hao wanaotetewa na mawakili, John Mapinduzi na Hudson Ndusyepo tayari wamekwisha kukaa mahabusu mwaka mmoja na nusu kutokana na zuio la dhamana lililowekwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), pamoja na madai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika.
Wakili Nchimbi akisoma hati ya mashtaka alidai kati ya Oktoba mosi na Novemba 13, 2013, katika maeneo tofauti ya Kinondoni, Dar es Salaam na Mjini Magharibi, Zanzibar, washtakiwa kwa pamoja walikula njama za kumiliki nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo, kinyume cha sheria.
Nchimbi alidai katika kipindi hicho cha Oktoba mosi na Novemba 13, 2013 katika maeneo tofauti ya Kinondoni, Dar es Salaam na Mjini Magharibi, Zanzibar washtakiwa hao kwa hiari waliratibu na kusimamia bila ya uhalali ukusanyaji wa nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo, vipande 1023 vyenye uzito wa kilogramu 2,915 na thamani ya Sh 7,480,125,000.
“Novemba 13, 2013 katika Bandari ya Zanzibar washtakiwa mlikutwa mnamiliki nyara hizo za Serikali bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori,”alidai.
Baada ya maelezo hayo, Nchimbi alidai sehemu kubwa ya upelelezi wa kesi hiyo umekwisha kukamilika na kwamba DPP ametoa kibali ambacho kinaipa mamlaka mahakama hiyo kuisikiliza kesi hiyo na akaomba ipangiwe tarehe waweze kukamilisha upelelezi.
Hata hivyo, Wakili Mapinduzi aliomba DPP aeleza maslahi ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa hao kwa mwaka mmoja na nusu watuhumiwa walichokaa mahabusu hadi sasa wanaposomewa mashtaka mapya ama aliondoe.
Hakimu alisema kwa mujibu wa sheria, hiyo inampa mamlaka DPP kuzuia dhamana anapoona inafaa na kwamba sheria hiyo ina changamoto zake na mahakama inaiheshimu huku akiutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi haraka haki ionekane inatendeka. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 2 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles