NAIROBI, KENYA
WAKATI Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake wa kiti cha urais Raila Odinga wakifunga kampeni zao juzi, vyama vyao kwa sasa vinatumia wamiliki wa baa, daladala kuhamasisha wapiga kura kabla ya uchaguzi wa kesho.
Katika mikutano hiyo miwili, viongozi hao walitoa wito kwa wafuasi wao wajitokeze kwa wingi ili kesho Jumanne wahakikishe ushindi katika raundi ya kwanza.
Rais Kenyatta na Odinga kwa sasa wanahakikisha wafuasi wao wanajitokeza kwa wingi ili kupata ushindi wa asilimia 50+1 ya kura.
Lakini pia ilifahamika kwamba kila upande kipindi hiki ambacho kampeni zimefungwa unashirikisha wamiliki wa baa, wahudumu wa matatu (daladala), wenye maduka na wamiliki wa vilabu vya burudani kuhakikisha kuwa wanatimiza lengo lao hilo.
Kutokana na mikakati hiyo, wachanganuzi wa mambo wanasema huenda idadi ya wapigakura watakaojitokeza kwa uchaguzi wa mwaka huu ikawa ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya taifa hili.
Naibu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Jubilee, David Murathe alisema watakumbatia mfumo wa ‘nyumba kumi’ kuwahimiza wapigakura katika ngome zao wajitokeze kwa wingi.
“Tumewashirikisha jumla ya watu 500,000 kutoka kila kijiji ambao wamejitolea kutusaidia kufanikisha lengo hili. Hii ni mbali ya mawakala wetu 45,000 katika vituo vya kupiga kura ambao kazi yao itakuwa ni kuhakikisha Jubilee inashinda,” Murathe alisema.
Kwa mujibu wa Murathe, makundi hayo ya watu waliojitolea yatashirikiana na mawakala wa Jubilee hadi kesho saa nane mchana kuhakikisha kuwa waliosalia vijijini, wagonjwa au walemavu wanasafirishwa kuenda kupiga kura.
Naye Afisa Mkuu wa NASA, Norman Magaya, alisema kila kamati ya watakaoshika doria katika vituo vya kura watapewa nakala ya orodha ya wapigakura kuhakikisha kuwa kila mtu anafika kupiga kura.
“Katika kila kamati, kuna mtu anayehusika na usafirishaji wa watu kutoka maeneo ya mbali hadi kituoni. Aidha, atahakikisha kuwa walemavu, wakongwe na wagonjwa wanasaidiwa,” alisema.
Mshiriki wa mpango huo katika eneo la Nyanza, Ruth Odinga alisema NASA itahakikisha wanachama wa kamati hizo wanapata chakula na marupurupu ili kuwapa moyo na kuhakikisha kuwa kila mpigakura anajitokeza.
Kwa mujibu wa wafuatiliaji wa uchaguzi huo, mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi wa kesho atapatikana kutokana na idadi ya wapigakura watakaojitokeza katika ngome za mirengo miwili.