27.6 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

‘KIFO CHA SOKOINE KILIKUWA TETEMEKO KWA FAMILIA’

Na ELIYA MBONEA-MONDULI


MTOTO wa pili wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Moringe Sokoine, Balozi Joseph Sokoine, amevunja ukimya na kuweka wazi kuwa kifo cha baba yao kilikuwa ni tetemeko kwa familia, Wilaya ya Monduli na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo aliitoa jana kijijini kwao Enguik Monduli Juu wilayani hapa wakati wa kumbukumbu ya miaka 33 tangu kifo cha kiongozi huyo kilipotokea kwa ajali ya gari Aprili 12, mwaka 1984 eneo la Dumila mkoani Morogoro.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya familia Balozi Sokoine alisema, familia imeendelea kusimamia misingi ya mambo yote aliyokuwa akifanya baba yao kwa nchi, Watanzania na familia yake.

“Mkuu wa wilaya hapa katika maelezo yake amesema kifo cha Sokoine kilikuwa pigo, lakini mimi naomba niseme kwamba halikuwa pigo tu, lilikuwa tetemeko kwa familia, wilaya yetu na Taifa.

“Kama ambavyo imekwisha elezewa na waliotangulia, Hayati Sokoine alijitoa kwa taifa na jamii, tumeelezwa pia alishika sana dini, mambo haya na mengine yamekuwa nguzo kwetu familia," alisema.

Katika salamu hizo kwa waombolezaji, Balozi Sokoine alitumia pia fursa hiyo kulishukuru Kanisa na Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano wao mkubwa kwa familia hiyo kila mwaka wanapokuwa na kumbukumbu hiyo.

Kwa upande wake Askofu Msaidizi Jimbo Kuu Katoliki la Arusha,  Prosper Lyimo,  akizungumza wakati wa kuongoza Misa ya kumbukumbu ya miaka 33 nyumbani hapo alisema, kiongozi huyo hatasaulika kwenye mioyo ya Watanzania.

“Zipo sababu zinazotufanya tuzidi kumwombea na kumkumbuka kwanza ni kujitoa kwake kuwatumikia watu kwa upendo, haki na hekima. Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya Sokoine.

“Mungu huwapokea watu na viongozi wanaojitoa kwa ajili ya maisha ya wengine, na katika hili ndivyo ilivyokuwa kwa Hayati Sokoine," alisema Askofu Lyimo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyekuwa mgeni rasmi katika kumbukumbu hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe,  alisema Hayati  Sokoine ataendelea kukumbukwa kila siku kutokana na matendo aliyoyafanya kwa Watanzania.

“Sokoine alitufundisha tufanye kazi, na hii leo ndio maana hata kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza kufanya kazi,”  alisema Maghembe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles