26.9 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, UJUMBE EU WATETA

Na Mwandishi Wetu – dar es salaam


RAIS Dk. John Magufuli ameshukuru nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kwa kutoa msaada wa Sh bilioni 500 (Euro milioni 205) kwa maendeleo kwa kipindi cha miaka minne.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Magufuli alifanya mazungumzo na Balozi wa EU, Roeland Van de Geer jijini Dar es Salaam jana.

Rais Magufuli alisema kutolewa kwa fedha hizo kumethibitisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na umoja huo.

Taarifa hiyo ilisema EU inatarajia kutoa fedha nyingine kiasi cha Euro bilioni 1.3 sawa na Sh trilioni 3 kuendeleza viwanda, kilimo na uzalishaji.

“Nimefurahi sana kwa uhusiano na ushirikiano wetu kushughulikia mambo ya msingi kwa Watanzania, nakuhakikishia kuwa fedha mnazozitoa zitatumika vizuri na zitatoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Balozi wa EU, Van de Geer alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi wake na dhamira yake ya kujenga uchumi na kusimamia utawala ubora, ikiwamo mapambano dhidi ya rushwa.

Pia, Van de Geer aliahidi kuwa nchi wananachama wa EU zitaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania.

Kwa upande mwingine, Rais Magufuli alifanya mazungumzo na Balozi wa Israel nchini, Yahel Vilan na alimhakikishia kuwa Tanzania imedhamira kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika masuala ya uwekezaji, biashara, utalii na uboreshaji wa huduma za kijamii.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Vilan aliahidi kujenga jengo la wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma mwishoni mwa mwaka huu.

“Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo, ikiwamo ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi,” alisema Vilan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles