Na Mwandishi Wetu-DODOMA
MSIMAMIZI wa Uchaguzi wa kupata wabunge wa Afrika Mashariki, Dk. Thomas Kashilillah, jana aliwarejesha wagombea wote wa Chadema na CUF katika kinyang’anyiro hicho.
Uamuzi huo umekuwa ni tofauti na ule alioutangazwa juzi ambako alisema vyama hivyo havijakidhi vigezo vya kuteuliwa kutokana na kutozingatia mgawanyo wa jinsia.
Alisema kwa upande wa CUF, wagombea wake waliruhusiwa kuwania nafasi hiyo kwa kuzingatia kigezo kwamba wote ni wanachama halali wa chama hicho baada ya kupata uthibitisho kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa upande wa Chadema, alisema majina ya wagombea wake yalirudishwa baada ya kukubalina na sababu zilizotolewa na chama baada ya kupewa barua juzi ya kufanya marekebisho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzingatia suala la jinsia.
Baada ya maelezo hayo wagombea hao walijinadi kila mmoja na kuuulizwa maswali kwa mujibu wa utaratibu.
Hata hivyo baada ya maelezo hayo, uliibuka mvutano kati ya kiti cha Spika na wabunge wa upinzani waliokuwa wanapinga kuingizwa orodha ya wajumbe kutoka CUF ya Mwenyekiti anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Wagombea waliojieleza jana na kupigiwa kura kulingana na makundi yao kwa CCM ni Wanawake Tanzania Bara: Zainabu Kawawa, Happiness Lugiko, Fancy Nkuhi na Happiness Mgalula na kwa upande wa wanaume Dk. Ngwaru Maghembe, Adam Kimbisa, Anamringi Macha na Makongoro Nyerere
Kwa upande wa CCM Zanzibar wanawake ni Maryam Ussi Yahya na Rabia Abdallah Hamid huku wanaume ni Abdallah Hasnu Makame na Mohammed Yussuf Nuh.
Chadema walioteuliwa ni Lawrance Masha na Ezekiah Wenje huku upande wa CUF Maalim aliyeteuliwa ni Wakili Twaha Taslima na upande wa CUF Lipumba ni Mohamed Habib Mnyaa, Thomas Malima ambaye alijitoa dakika za mwisho pamoja na Sonia Magogo.