26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

UKIJIKUBALI UTAJIFUNZA KUKUBALI KUMUACHA AENDE…

sad-woman

NAKUMBUKA mwaka 2012, majira kama haya nilipata mgeni ofisini kwangu. Nakumbuka vizuri sana, ilikuwa Desemba 27, siku mbili baada ya Sikukuu ya Krismas na siku nne kabla ya mwaka mpya wa 2013.

Alikuwa binti aliyeonekana kuwa mrembo, lakini aliyekongoroka. Afya yake haikuwa sawa sana, lakini mimi wakati huo nilikuwa mgonjwa.

Nilikuwa ndiyo kwanza nimetoka Muhimbili ambapo nilifanyiwa upasuaji. Kwa maneno mengine, mimi ndiye nilikuwa mgonjwa, lakini yeye aliyekuwa mzima alionekana kama mgonjwa!

Uso wake haukuwa na tabasamu, macho yake yalilazimisha kuangaza, lakini kila alipofungua kinywa na kuzungumza, yalidondosha machozi. Nilikuwa sijapona vizuri, lakini niliamua kujikongoja hadi ofisini ili nizungumze naye kutokana na ‘usumbufu’ aliokuwa akinipa mara kwa mara.

Haukuwa usumbufu hasa, ila alikuwa akinitafuta sana, akinieleza namna anavyoteswa na mapenzi. Nilijitahidi  kumtuliza, lakini ilishindikana. Baadaye nikahiyari azungumze na machozi yake. Akaongea huku akilia.

Alikuwa kwenye uhusiano na kijana waliyekutana chuo. Wakati huo, huyo binti alikuwa na miaka 24 (sasa 28), akiwa anafanya kazi ya muda kwenye kampuni moja ya simu za mkononi jijini Dar.

Jamaa yake alikuwa mwajiriwa serikalini. Kwa maelezo yake, huyo jamaa alimtangulia chuo, kwahiyo wakati anamaliza, yeye ndiyo alikuwa akikaribia kuingia mwaka wa pili.

Tatizo ni vitimbi vya huyo jamaa. Hebu ngoja hapa nimpe jina bandia Ben na huyo dada nimwite Diana: Ben alikuwa na vituko visivyo na kawaida. Ilikuwa si ajabu kukuta meseji za wanawake mbalimbali kwenye simu yake akizungumza nao mambo ya mapenzi.

Kila mwanamke kwa nafasi yake, kwake alikuwa baby, sweetie, darling na majina mengine ya namna hiyo. Diana akajitahidi kuvumilia kwa sababu eti alikuwa ANAMPENDA SANA!

Alinieleza mengi. Mambo mengi yasiyovumilika. Kwa maelezo yake, ni kwamba Ben hakuwa na mapenzi kabisa na Diana. Alikuwa akijiridhisha tu. Hakuwa na nia ya dhati, lakini Diana alimpenda kwa dhati.

Diana aliniambia alikuwa na uhakika kwa asilimia mia moja kuwa HAPENDWI, lakini aliamua KUVUMILIA tu kwa sababu alishindwa kabisa KUMUACHA!

 

USHAURI UKAANZIA HAPO

Nilimpa maneno ya ujasiri, nikamweleza thamani ya moyo wake, thamani ya maisha yake na namna ambavyo ni hatari kuuchezeachezea moyo wake.

Eti anasema hawezi kumuacha, kwani alikaa naye tumboni mwa mama yake? Tatizo kubwa la Diana lilikuwa ni kujikubali. Alikuwa haamini nje ya Ben. Kwamba hakuna mwanaume mwingine atakayemuelewa zaidi ya  Ben.

Nilimweleza wanaokataa kuachana na maumivu, maana yake hawaamini kama wanaweza kupata mwingine; tafsiri hapo ni moja tu, HAKUJIKUBALI!

Eti jamaa alikuwa akimwambia nenda tu… lakini ipo siku utanikumbuka. Amkumbuke yeye ni mama yake? Anajua uchungu wake? Anajua wakati wazazi wake wanateseka kumlea?

Nikamwambia amuache aende zake, maisha yalikuwa mbele yake. Ulionekana kama ushauri wa kikatili, lakini uliokuwa na maana. Niliachana na Diana akitabasamu, tukaagana kwa furaha akiniahidi kufanyia kazi ushauri wangu.

Sikuwasiliana naye tena baada ya pale.

 

KWANINI NIMEANDIKA LEO?

Jioni ya Jumamosi iliyopita, nilikuwa Mlimani City. Nilipita pale kwa mahitaji yangu. Wakati naingia kwenye lango kuu, nikasikia mtu ananiita kwa jina. Nilishtuka kidogo na kusimama.

Nikakutana na watu wawili – mwanaume na mwanamke wakiwa na mtoto mdogo kwenye bebeo la matairi – mwanaume anamsukuma. Sikuwafahamu.

Tulisalimiana kwa kushikana mikono. Yule mwanamke akaniuliza kama namkumbuka, nikamwambia hapana. Akasema yeye ndiye Diana. Alinisimulia vizuri, nikamkumbuka.

Yule mwanaume ni mume wake wa ndoa yenye miaka miwili. Kwamba aliachana na Ben na kubaki mwenyewe, lakini miezi michache baadaye, akajitokeza huyo jamaa ambaye sasa ndiye mume wake.

Walianza uhusiano, taratibu za uchumba zikafanyika, kisha mwezi Januari 2014 wakafunga ndoa.

Tutajadili vizuri Jumamosi ijayo, kuna kitu kikubwa kitabadilisha fikra zako kwenye uhusiano mwaka huu 2017. Naenda zangu kuogelea baharini.

 

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, aliyeandika vitabu maarufu True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA MAISHA YA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles