MARKUS MPANGALA NA MTANDAO
JANUARI 20 mwaka huu, Rais mteule kutoka Chama cha Republican, Donald Trump, anatarajiwa kuapishwa rasmi kuwa rais wa Marekani, akichukua nafasi ya Barrack Obama wa chama cha Democrat anayemaliza muda wake.
Tangu kuchaguliwa kwake mnamo Novemba 8 mwaka jana, Trump amekuwa akifanya uteuzi wa wanasiasa na wataalamu mbalimbali kuwa sehemu ya baraza lake la mawaziri na maeneo mengine. Makala haya yanaelezea wateule wake wanavyotazamwa nchini humo na ulimwenguni kwa ujumla.
REINCE PRIEBUS
Donald Trump amemteua mwenyekiti huyo wa Kamati ya Taifa ya chama cha Republican, kuwa Katibu Kiongozi wa Ikulu. Priebus (44) ana uhusiano wa karibu na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Paul Ryan.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema uteuzi wa Piebus umewaudhi wafuasi wake wa hali ya chini na hii inaashiria kwamba, uongozi ujao unalenga kufanya kazi kwa karibu na Bunge la Kongresi kujihakikishia ushindi wa mapema wa baraza hilo.
Jukumu la mkuu wa wafanyakazi ni pamoja na kuruhusu na mtengeneza ajenda kwa rais, na kwamba ni mmoja wa chaguo muhimu la mapema kwa Trump.
STEPHEN BANNON
Miongoni mwa majina yaliyowashtua Wamarekani ni Stephen Bannon (63), ambaye alikuwa ni mwenyekiti wa Taasisi ya Breitbart News, ambayo ni tovuti yenye maoni ya mrengo wa kulia. Bannon ameteuliwa kuwa mkuu wa mipango na mshauri mwandamizi katika timu ya rais.
Baada ya uteuzi wa wawili hawa, Rais Trump alisema ni viongozi wenye sifa za hali ya juu waliofanya kazi pamoja wakati wa kampeni zake za kuingia Ikulu ya Marekani.
PETER NAVARO
Profesa huyo (67) anajulikana kuwa mkosoaji mkubwa wa China, ameteuliwa kuongoza Baraza la Taifa la Biashara la Ikulu ya Marekani ambayo ni ofisi mpya itakayosimamia masuala ya biashara pamoja na sera za viwanda, ikiwa ni moja ya mipango ya rais huyo mteule kufanya mageuzi katika sera ya uchumi ya Marekani.
Navaro ndiye mwandishi wa kitabu cha Death by China. Serikali ya China kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, imekosoa vikali uteuzi huo kwa madai unaharibu uhusiano wa mataifa hayo mawili, huku ikikumbukwa Navaro anaiunga mkono Taiwan kuwa taifa huru nje ya China. Ni profesa wa Chuo Kikuu cha California.
REX TILLERSON
Uteuzi wa Trump umeonekana kuwalenga wafanyabiashara mabilionea ambapo katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje ameteuliwa Rex Tillerson (64).
Waziri Tillerson anatajwa kuwa na uhusiano wa karibu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, jambo ambalo limewatia wasiwasi baadhi ya wanachama wa vyama vya Democratic na Republican.
Tajiri huyo wa mafuta kutoka Texas ni mwenyekiti na mtendaji mkuu wa kampuni ya mafuta ya ExxonMobil, hana ujuzi wowote wa kidiplomasia lakini ana uhusiano mkubwa wa biashara katika nchi nyingi za dunia, hasa Urusi na Msumbiji. Tillerson, mwenye umri wa miaka 64, ni mhandisi wa majengo na alijiunga na Exxon baada ya kumaliza masomo yake Chuo Kikuu cha Texas.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema huenda uteuzi wa Tillerson ambao utathibitisha Baraza la Seneti atakabiliana na utata katika machakato huo ikihofiwa huenda atakataliwa na baraza hilo, huku akitajwa kutokuwa na uzoefu wowote. Uteuzi wake umesababisha mgawanyiko kwenye timu ya rais mteule.
JAMES MATTIS
Jina la Jenerali huyu mstaafu lilichekesha na kushtua mno, lakini ndiyo hali halisi inayotokea chini ya rais mpya. Trump amemteua Jenerali Mattis (66) kuwa waziri mpya wa ulinzi. Mattis ni maarufu duniani kwa jina la ‘Mad Dog’, ni mwanajeshi wa zamani aliye na sifa ya kuweka mikakati, kuwa na msimamo mkali na mpinzani mkubwa wa Iran.
Trump alimfananisha James Mattis na Jenerali George Patton, kamanda wa jeshi la Marekani kwenye Vita Kuu ya Pili ambapo wenzake walimpa jina la ”Old Blood-and-Guts” kutokana na ujasiri wake.
WILBUR ROSS
Uteuzi wa mabilionea unaendelea ambapo katika orodha hiyo yumo Wilbur Ross (78). Ross ameteuliwa kuwa waziri wa biashara katika kipindi cha utawala wa Trump.
Ross ni mwenyekiti wa kampuni binafsi ya W.L.Ross &Co ambayo inafahamika kwa kununua makampuni yaliyoshindwa kujiendeleza kibiashara.
NIKKI HALEY
Huyu ni Gavana wa Jimbo la South Carolina, ambaye ameteuliwa kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa. Haley (44), gavana wa mihula miwili katika jimbo hilo, ni mwanasiasa anayetokana na wazazi wahamiaji kutoka nchini India. Ni mwanamke wa kwanza kuteuliwa na Trump.
BETSY DEVOS
Pia rais huyo mteule alimteua Betsy Devos (54) kuwa Waziri wa Elimu. Devos ni mwanamke wa pili kuteuliwa katika safu ya uongozi wa Trump baada ya Nikki Haley, ambapo katika orodha ya baraza la mawaziri limejaa wanaume. Mwanamama huyu ni mkwe wa Richard DeVos, mmiliki wa kampuni ya Amway na mwenye utajiri wa Dola bilioni 5.1 za Marekani.
ELAINE CHAO
Ni mwanasiasa wa Kimarekani aliyezaliwa huko Taipei, Taiwan nchini China. Chao ni mwanasiasa wa kwanza mwanamke mwenye asili ya Asia na Mtaiwani wa kwanza kuteuliwa kuwa waziri wa usafirishaji katika historia ya Marekani.
BEN CARSON
Licha ya kuwa mshindani wake ndani ya Republican, Donald Trump amemteua Ben Carson (65) kuwa Waziri wa Makazi na Ustawi wa Miji. Ben Carson alistaafu kazi ya udaktari wa upasuaji wa kichwa, anatajwa kuwavutia wafuasi wa chama cha Republican.
RICK PERRY
Alikuwa miongoni mwa walioomba kuteuliwa kugombea urais ndani ya chama cha Republican, baadaye alimuunga mkono Trump. Perry, mwenye umri wa miaka 66, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nishati.
TOM PRICE
Ameteuliwa kuwa Waziri wa Afya na huduma za binadamu katika Serikali ya Trump. Price, mwenye miaka 62, amekuwa mbunge wa Kongresi akiwakilisha Jimbo la Georgia na ni mtaalamu wa upasuaji wa mifupa ambaye amekuwa akiongoza kamati ya bajeti katika Bunge la Wawakilishi.
Aliwahi kukabidhiwa jukumu muhimu katika mipango ya chama cha Republican wa kupinga mpango wa bima ya afya ulioanzishwa na Rais Obama.
JOHN F. KELLY
Ameteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Marekani. Kelly amewahi kuwa mwanajeshi aliyefikia cheo cha jenerali. Ana umri wa miaka 66.
RYAN ZINKE Â
Ni Mbunge wa wawakilishi wa Republican kutoka Jimbo la Montana, ambaye alikuwa mwanajeshi wa Kikosi Maalumu cha Majini (Navy Seal). Ameteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani. Ana umri wa miaka 55
STEVEN MNUCHIN
Ateuliwa kuwa Waziri wa Fedha, ni mjuzi wa uwekezaji, na uendeshaji wa biashara ya fedha nchini humo. Ana umri wa miaka 54. Naye ni miongoni mwa mabilionea walioteuliwa kuwa mawaziri wa Trump.