Na MALIMA LUBASHA -SERENGETI
FAMILIA ya watu watatu wa Mtaa wa Chamoto, Kata ya Stendi Kuu, Tarafa ya Rogoro wilayani Serengeti mkoani Mara, wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuwafanyia ukatili watoto wawili wa kike kwa njia ya ukeketaji.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Pascal Nkenyenge, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya, Amaria Mushi, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Ikwabe Charali (32), Robi Petro (31) wakazi wa Chamoto na Nyangi Charali (35) mkazi wa Kijiji cha Matare wilayani hapa.
Alisema washtakiwa hao ambao ni baba, dada na mke wa mshtakiwa wa kwanza Ikwabe, wanatuhumiwa kuwafanyia ukatili watoto wa kike kwa kuwakeketa Desemba 19, mwaka huu ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka mawili yanayowakabili katika kesi hiyo, walikana kuhusika na tukio hilo kwani walitenda kosa hilo.
Hakimu Mushi, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 2, mwakani itakapotajwa tena hivyo kuamuru washtakiwa warudishwe mahabusu.
Wakati huo huo, Mkazi wa Kijiji cha Bonchugu, Kata ya Manchira wilayani Serengeti mkoani Mara, Chacha Matiko (53), amehukumiwa na mahakama hiyo kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh 800,000 baada ya kupatikana na makosa ya kuingia ndani ya Hifadhi ya Serengeti na kuchunga ng’ombe bila kibali.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ismael Ngaile.
Alisema mahakama imetoa adhabu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.