Na FARAJA MASINDE,
SASA HIVI kuna wimbi kubwa zaidi la wanafunzi ambao wanatafuta nafasi ya kwenda kusoma kwenye vyuo vikuu nje ya nchi.
Katika kutathmini viwango vya elimu duniani, wengi wamekuwa wakiangazia zaidi ubora wa vyuo, huku lile la mataifa gani ambayo yanafanya vyema kitaaluma likiwa halizingatiwi na wazazi na hata wanafunzi wenyewe wanaotaka kwenda kusoma.
Kila siku, kila mwezi, kila mwaka tafiti mbalimbali zinafanyika kuhakikisha kuwa kunaendelea kuwapo na utofauti wa vyuo bora na vile vinavyoshika nafasi ya mwisho kitaaluma.
Hata hivyo, mashirika hayo ya utafiti yameenda mbali zaidi kwa kuleta matokeo ya utafiti juu ya vyuo vikuu vyenye wanafunzi welevu zaidi duniani.
Kitu cha kipekee kwenye utafiti huo ni kwamba kumekuwa na mabadiliko makubwa zaidi ikilinganishwa na matokeoya mashirika mengine yanayofanya tafiti za vyuo vikuu.
Shirika la Kimataifa la Uchumi na Maendeleo (OECD) limetoa matokeo ya mtihani wa kupima uwezo wa wanafunzi wanaohitimu kutoka nchi mbalimbali.
Orodha ya ubora wa vyuo vikuu hutawaliwa na vyuo vikuu kutoka Marekani na Uingereza kama vile Harvard, MIT, Stanford, Oxford, Cambridge na UCL.
Lakini baada ya OECD kuchunguza uwezo wa kusoma na kuandika miongoni mwa wahitimu kutoka vyuo vikuu, wanafunzi walio bora zaidi ilibainika wanatoka Japan na Finland na wala si Marekani na Uingereza.
Mwezi uliopita shirika hilo la OECD limetaja mataifa 10 yanayotoa wanafunzi bora zaidi, wanaohitimu masomo yao kwenye vyuo hivyo kuwa ni pamoja na Japan, Finland, Uholanzi, Australia na Norway.
Mataifa mengine yenye wanafunzi bora duniani ni pamoja na Ubelgiji, New Zealand, England, Marekani na Jamhuri ya Cheki.
Mataifa hayo yote huwa mara nyingi hayaingizi chuo hata kimoja kwenye orodha ya vyuo vikuu 10 bora duniani kwenye tafiti mbalimbali zinazofanywa na mashirika ya utafiti.
Badala ya vyuo vikuu vya Marekani kufana, yamkini vyuo vikuu vya Norway na Australia vina wanafunzi bora wanaohitimu.
Kwa mujibu wa orodha ya ubora wa vyuo ya QS World University Rankings, kulikuwa na vyuo 32 vya Marekani katika 100 bora na chuo kikuu kimoja pekee kutoka New Zealand.
Lakini ripoti ya OECD inaonesha kuwa wanafunzi wa New Zealand wanafanya vyema kushinda wenzao Marekani.
Hata hivyo, tafiti hizi zinazofanywa na mashirika haya mbalimbali zimekuwa zikitofautiana kwa kiwango kikubwa ambapo si ajabu kuona leo chuo kikishika nafasi ya kwanza kwa ubora kwenye utafiti wa QS lakini kikashindwa kuingia hata kwenye 10 bora za OECD au hata ule wa shirika la utafiti wa vyuo vikuu la THE.
Kwa mujibu wa utafiti wa shirika la QS inaonyesha kuwa vyuo vikuu bora duniani ni Massachusetts Institute of Technology (MIT), Chuo Kikuu cha Stanford, Harvard, Cambridge na Taasisi ya Teknolojia ya California (Caltech).
Vingine vilivyoko kwenye 10 bora katika utafiti huo ni Chuo Kikuu cha Oxford, London, ETH Zurich, Imperial College London huku nafasi ya mwisho ikinyakuliwa na Chuo Kikuu cha Chicago kilichopo nchini Marekani.