Na BENJAMIN MASESE,
WANANCHI wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria wameaswa kuacha kuchota au kutumia maji yenye rangi ya kijani na maziwa.
Mtaalamu wa Usimamizi wa Misitu wa Mradi Hifadhi ya Mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria (LVEMP II), Simon Msemwa amesema maji hayo yamepoteza ubora wake kutokana na kuzidiwa na uchafu wa unaotokana na kinyesi na kemikali.
Alikuwa akizungumza na Kamati ya Mahesabu ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) ilipotembelea miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Msemwa alisema vitu vinavyochangia maji ya Ziwa Victoria kuchafuka ni shughuli za binadamu zikiwamo uvuvi haramu, kilimo pembeni mwa ziwa na ujenzi wa makazi ya watu karibu na mito au ziwa.
Sababu nyingine ni mafuta ya vyombo vya usafiri wa majini, kemikali kutoka viwandani na utupaji ovyo wa takataka ngumu.
Msemwa alisema zipo sehemu pembeni mwa Ziwa Victoria maji yake yamefikia hatua ya kubadilika na kuwa na rangi ya kijani au maziwa kutokana na uchafu .
Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiyatumia kwa matumizi mbalimbali jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
“Naombeni kuwaomba wananchi kuacha kutumia maji yenye rangi hizo kwa sababu yanakuwa na uchafu uliozidi, maana ipo migodi, viwanda na shughuli zingine za kilimo hususan bustani ambazo mara nyingi hutumia dawa.
“Katika vyombo vya usafiri vimekuwa miongoni mwa vitu vinavyochafua maji, mfano meli za zamani hazina mfumo wa kuhifadhi taka.
“Kwa sababu hiyo kinyesi huingia moja kwa moja majini …ndiyo imefikia hatua ya Sumatra kuja na sheria ya meli mpya kuwa na kontena la taka,”alisema.