26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tiba ya Ukimwi yanukia

Mtafiti akiwa kazini
Mtafiti akiwa kazini

Na JOSEPH HIZA,

TANGU kugundulika kwa ugonjwa wa Ukimwi maradhi hatari yasiyo na tiba zaidi ya miongo mitatu iliyopita, wanasayansi kote duniani wamekuwa wakikesha kutafuta tiba ya kukabiliana nao bila mafanikio.

Lakini kadiri muda unavyokwenda na teknolojia kukua, uelewa wetu wa namna virusi vya Ukimwi (VVU) vinavyoambukizwa, vinavyoishi na kusababisha madhara ndivyo unavyozidi kuongezeka.

Sehemu ya mafanikio ya uelewa huo ni upatikanaji wa dawa zinazozuia maradhi hayo kuendelea kuenea na kuleta madhara ya kiafya mwilini mwa aliyeambukizwa, yaani dawa za kufubaza makali ya virus vya Ukimwi (ARVs).

Changamoto kuu hadi sasa ni upatikanaji wa dawa ambayo inaweza kuua kabisa VVU kutoka katika damu ya mtu anayeishi navyo.

Katika harakati hizo za kupata tiba mujarabu, wanasayansi wamekuwa wakikabiliwa na kikwazo kikubwa kinachozuia upatikanaji wa dawa hizo.

Tangu kugundulika kwa VVU hadi leo hii, sababu kuu inayozuia upatikanaji wa tiba itakayoweza kuviua kabisa virusi hivyo au upatikanaji wa kinga ya kuvizuia kuingia kwenye mwili na kuleta madhara inatambulika kuwa ni uwezo wake mkubwa wa kubadilika na kujenga kuta zinazozuia dawa isiweze kufanya kazi ya kuvidhuru.

Uwezo huo wa VVU, umekuwa changamoto kubwa inayozuia dawa zote zilizowahi kutengenezwa kwa ajili ya kuviua kushindwa kufanya kazi hiyo.

Wanachofanikiwa watafiti wengi katika majaribio yao ni kuviondoa virusi kutoka damu lakini baada ya muda wanakuta vimerudi.

Ni hapo katika uchunguzi wao walikuja kubaini kuwa seli za VVU zina tabia hiyo ya kujifichaficha.

Miongoni mwa maeneo vinakopenda kujificha ni pamoja na katika ubongo, uti wa mgongo, utumbo na kadhalika.

Hivyo mkazo ukawa namna ya kuviamsha na kuvivuta virusi hivyo kutoka mafichoni na kujitokeza sehemu ya wazi kwa ajili ya kuangamizwa.

Lakini kwa sasa wanasayansi wa Uingereza wanaeleza matumaini kuwa hatimaye tiba i karibu kupatikana, ikiwa na uwezo wa kukabili ujanja wa VVU kujificha.

Ni baada ya majaribio yao miongoni mwa watu 50 wenye maradhi hayo kuonesha mafanikio kwa Mwingereza aliyekuwa amekamilisha mchakato wa matibabu.

Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 44, ambaye jina lake limehifadhiwa alionekana hana VVU katika damu yake, baada ya awali kupimwa na kuthibitika kuwa na VVU.

Iwapo majaribio zaidi yataonyesha kuwa damu ya Mwingereza huyo iko huru na VVU, atakuwa mtu wa kwanza duniani kupona kabisa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa gazeti la Telegraph la Uingereza, kile wanachosema wanasayansi kinaweza kuwa jibu la VVU, ni tiba mpya iliyotengenezwa na timu ya watafiti kutoka vyuo vikuu tofauti nchini Uingereza.

Matibabu hayo yamelenga kuondoa kabisa VVU vilivyojificha ndani ya mwili wa binadamu.

“Haya ni moja ya majaribio ya kwanza makini yaliyolenga kutibu kabisa VVU,” alisema Mark Samuels, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utafiti wa Afya kwa ajili ya miundombinu ya tafiti za kitabibu nchini humo.

“Tunasaka njia ya kweli ya kutibu VVU. Hii ni changamoto kubwa na bado ni mapema lakini maendeleo yaliyopatikana ni makubwa.”

Vyuo vikuu vilivyohusika katika mchakato huo na tafiti zinazohusisha majaribio hayo ni pamoja na; Oxford, Cambridge, Imperial College London, Chuo Kikuu cha London na Chuo cha Mfalme London.

Mwingereza huyo, ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sasa ni mfanyakazi wa sekta ya kijamii wa jijini London.

“Itakuwa habari njema sana iwapo uponyaji utakuwa umetokea. Mara ya mwisho nilichukuliwa vipimo vya damu wiki chache zilizopita na hakukuonekana uwapo wa virusi,” alisema.

Kwa mujibu wa Profesa Sarah Fidler wa Chuo cha Imperial London, matibabu maalumu yanayoaminika kuwa kuwa tiba ya VVU yanaaminika kuviondoa kabisa mwilini.

Sababu inayowafanya waamini kwamba tiba i karibu ni kwa vile matibabu hulenga seli zilizolala pia, yaani ambazo hujificha.

Kwa mujibu ya wanasayansi, tiba hiyo hulenga kuangamiza VVU katika kila sehemu ya mwili wa mwanadamu na inafanya kazi kwa kuunganishwa na chanjo.

Waathirika kwanza hupatiwa chanjo ili kuupa mfumo wa kinga uwezo wa kuzitambua seli zilizoathirika na kuzitoa na kisha dawa mpya iitwayo Vorinostant hutumika.

Dawa hiyo mpya huhuisha VVU vilivyojificha ili vionekane kwenye mfumo wa kinga na kuangamizwa.

Ni kupitia seli zilizoathirika ambazo ghafla hujitokeza kutoka maficho yao na mfumo wa kinga uliopewa nguvu huziangamiza.

Kwa sasa dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs) huzuia tu VVU kuzaliana lakini haziweza kuziangamiza.

Wanasayansi wanaofanya kazi katika majaribio na tiba wanasisitiza ni muhimu kwa sasa watu wahesabu tu kwamba tiba i karibu, si kuwa imepatikana.

Wanasayansi walioona namna tiba hiyo inavyofanya kazi katika maabara na hawana sababu ya kudhani kuwa haitofanya kazi katika miili ya binadamu.

Hata hivyo, bado wanaendelea kuifanyia majaribio kabla ya kuthibitisha kuwa inatibu mtu na kuwa salama dhidi ya VVU katika damu yake.

Leo hii kuna watu milioni 37 wanaoishi kwa VVU duniani achilia mbali wale waliokwishafariki dunia na takwimu zinaonesha kwamba asilimia 17 ya watu hawa wanaoishi na maradhi hayo hawajui kama wameambukizwa.

Licha ya matumaini safari bado inaweza kuwa ndefu, subira inahitajika kwa watu kuendelea kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU na waathirika kufuata masharti kutoka kwa wataalamu wa afya ili kuendelea kuishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles