Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania jana imemhukumu kunyongwa hadi kufa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (SP), Christopher Bageni.
Baada tu ya kutolewa kwa hukumu hiyo, SP Bageni alipelekwa Gereza la Ukonga Dar es Salaam ambako alifikishwa majira ya saa 9:45 jioni kwa ajili ya kusubiri kutekelezwa kwa hukumu yake.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) akipinga aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na maofisa wenzake watatu akiwemo Bageni kuachiwa huru na Mahakama Kuu mwaka 2009.
Rufaa hiyo ilisikilizwa na kutolewa hukumu na jopo la majaji watatu, Jaji Benard Luanda, Sauda Mjasiri na Senistocles Kaijage.
Akisoma hukumu hiyo, Msajili wa Mahakama hiyo, John Kahyoza, aliwataja wajibu rufani kuwa ni Zombe, SP Bageni, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Urafiki, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ahmed Makelle na Rajabu Bakari.
Alisema Mahakama ya Rufaa ilipitia ushahidi uliotolewa Mahakama Kuu na kuona kwamba mahakama hiyo ilishindwa kuwatia hatiani washtakiwa kwa mauaji na kwa kosa la kusaidia mauaji kufanyika.
“Kosa la kuua na kosa la kusaidia kuua ni makosa mawili tofauti, si sahihi kwa mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji kutiwa hatiani kwa kosa lingine ambalo tangu mwanzo mshtakiwa alitakiwa kulijua ili aweze kujitetea.
“Makosa hayo si makosa yanayofanana hivyo mahakama hiyo ilitofautiana na hoja za upande wa Jamhuri kwamba washtakiwa watiwe hatiani kwa kosa la kusaidia kuua baada ya kushindwa kutiwa hatiani kwa mauaji.
“Washtakiwa wote katika utetezi wao walipinga kuhusika katika mauaji hayo lakini mjibu rufani wa nne Rajabu alisema ukweli katika ushahidi wake kwa kueleza tukio la mauaji lilivyofanyika katika Msitu wa Pande.
“Pamoja na mjibu rufani kusema ukweli lakini ushahidi wake ulitakiwa kupokelewa kwa makini na unatakiwa kuwepo na ushahidi mwingine wa kuunga mkono.
“Mjibu rufani wa kwanza mahakama haioni kama kuna ushahidi wa kumtia hatiani kwa mauaji wala kwa kusaidia kuua japo kuna jambo kichwani mwake analolifahamu kuhusu mauaji hayo, ushahidi mwingine unaonyesha wajibu rufani watatu walishuhudia mauaji lakini hawakuua,” linasema jopo.
Jopo lilisema wamekubaliana kwamba watu wanne waliuawa kwa bunduki na mauaji yalikuwa ya kinyama katika Msitu wa Pande.
Mahakama hiyo ilijiuliza maswali kwamba je, wajibu rufani walikuwepo Pande, jibu ni kwamba wajibu rufani 2,3,4 walikuwepo katika msitu huo na mjibu rufani wa nne alisema ukweli mahakamani kuhusiana na tukio hilo.
Ilidaiwa kwamba mauaji hayo yalifanywa na Polisi Sadi lakini mshtakiwa huyo hajawahi kushtakiwa lakini mahakama inajiuliza marehemu walipelekwa Pande kwa amri ya nani.
“Mahakama inajiuliza nini nia ya kuwapeleka marehemu Pande sehemu ambayo haina hata nyumba, mjibu rufani wa pili, Bageni ndiye alitoa amri ya kuua, ushahidi unaonyesha marehemu walipelekwa Pande na washtakiwa walikwenda Pande.
“Marehemu walipelekwa huko ili tukio la mauaji lifanyike bila kipingamizi kwa kibali cha Bageni, ushahidi wa mjibu rufani wa nne uliungwa mkono na tabia ya Bageni kwamba alikuwa akificha ukweli kuhusu mauaji hayo.
“Kulikuwa na ushahidi wa maofisa watatu wa polisi, wote walidanganya kwamba mauaji yalitokea Sinza katika majibizano kati ya Polisi na marehemu wakati wengine wa Sinza walisema hawakusikia tukio la aina hiyo kutokea.
“Mjibu rufani wa 1,3,4 rufani dhidi yao inatupwa hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani, mjibu rufani wa pili mahakama inatengua kuachiwa kwake kutiwa hatiani na Mahakama Kuu, inamhukumu kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya watu wanne,” alimalizia kusoma hukumu hiyo vilio vikatawala katika chumba cha mahakama.
Wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Morogoro waliouawa ni Sabinus Chigumbi maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi mkazi wa Manzese Dar es Salaam, Juma Ndugu.
Marehemu hao waliuawa kinyama kwa kupigwa risasi na taarifa ya awali iliyotolewa na polisi ilieleza kuwa walikuwa majambazi waliouawa katika majibizano ya risasi na polisi.
Hata hivyo, taarifa ilipingwa na watu wa karibu wa marehemu hao walioeleza kuwa walikuwa wafanyabiashara wa madini wenyeji wa Mahenge mkoani Marogoro na kwamba walifika Dar es Salaam kwa shughuli zao za kibiashara.
Baada ya kuwepo kwa mkanganyiko wa taarifa, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, aliunda Tume ya kuchunguza mauaji hayo iliyokuwa chini ya Jaji Mussa Kipenka ambayo nayo katika ripoti yake ilipingana na taarifa ya polisi.
Siku chache baada ya Rais Kikwete kupokea ripoti ya Tume ya Jaji Kipenka, Zombe na wenzake walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kushtakiwa kwa makosa ya mauaji lakini mahakama hiyo iliwaachia huru kabla ya Mkurugenzi wa Mashtaka kukata rufaa Mahakama Kuu.
Zombe na wenzake walidaiwa kutenda makosa hayo Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande, uliopo wilayani Kinondoni baada ya kuwakamata wafanyabiashara hao Sinza, walipokuja Dar es Salaam kuuza madini.