25.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaume 300,000 wafanyiwa tohara

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Bakari Mhina.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Bakari Mhina.

Na Pendo Fundisha, Mbeya

WANAUME zaidi ya 300,000 wenye umri kati ya miaka 10 na kuendelea, wamefanyiwa tohara mkoani Mbeya na Songwe ikiwa ni sehemu ya harakati za Serikali kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) nchini.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Bakari Mhina, alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa kondomu ya kiume ya Zana inayotolewa na Serikali.

Alisema idadi hiyo ni sawa na asilimia 80 huku lengo la Serikali ni kufanya tohara kwa wanaume wapatao 400,010 hadi kufikia mwakani ili kufikia asilimia 100.

“Tafiti zimebainisha kwamba asilimia kubwa ya wanaume ambao hawakufanyiwa tohara wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya magonjwa ya ngono ukiwamo Ukimwi na ndiyo sababu Serikali iliazimia kuendesha zoezi hili la tohara bila gharama yoyote.

“Kwa mujibu wa takwimu za utafiti uliofanyika nchini kabla ya Mkoa wa Mbeya kugawanywa, mkoa huo ulishika nafasi ya tatu kwa kuwa na maambukizi makubwa na ulikuwa na asilimia tisa, huku ukiwa umetanguliwa na mikoa ya Njombe wenye asilimia 14 na Iringa asilimia 9.1,” alisema.

Akizindua kondomu hiyo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika, alisema licha ya kondomu kupunguza maambukizi ya Ukimwi, pia zinasaidia kuepuka mimba zisizotarajiwa na aliwataka wahusika kuhakikisha wanazisambaza kwa walengwa.

“Kondomu hii ya Zana imezinduliwa Mbeya kutokana na kuonekana kuwa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha watu walioambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi,” alisema.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mratibu wa Afya Kitengo cha Ukimwi Mkoa wa Mbeya, Dk. Francis Phily, alisema hadi sasa mkoa umesambaza kondomu ya Zana milioni 1.5 katika wilaya mbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles