Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekiri kuwa mashine 250 zilizotumika katika zoezi la majaribio la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) lililofanyika mwezi uliopita katika majimbo matatu nchini, hazifai.
Imesema baada ya kugundua kasoro zilizo kwenye mashine hizo, sasa inakusudia kufanya marekebisho wakati wa utengenezaji wa mashine mpya 7,750 zinazotarajiwa kuagizwa kwa ajili ya kutumika katika kazi hiyo kuanzia mwezi ujao.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu tathimini ya utekelezaji wa majaribio ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR.
Jaji Lubuva alisema changamoto zilizojitokeza katika majaribio hayo ambayo yalihusisha watu 41,721 ni pamoja na matatizo ya programu za mifumo ya kompyuta.
Changamoto nyingine alizozitaja ni hali ya hewa ya joto ambayo iliharibu urahisi wa utendaji kazi wa mashine hizo pamoja na watumishi kutokuwa na ujuzi wa kuzitumia.
“Changamoto zilikuwa nyingi za kibinadamu na kimiundombinu hasa hali ya hewa ya joto kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro iliyosababisha baadhi ya mashine kushindwa kufanya kazi inavyotakiwa na hivyo kukwamisha shughuli za uchapaji kadi za kupigia kura,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema kompyuta mpakato zilizokuwa zikitumika katika kazi hiyo ziliwekewa bati la kuzuia zisiibiwe kwa urahisi lakini iligundulika baadaye kuwa bati hilo lilikuwa likizuia mzunguko wa hewa ndani ya mashine hizo.
Aidha, alieleza kuwa baadhi ya watendaji wa tume yake hawakuwa na ufahamu wa kutumia mashine hizo hivyo wanahitaji elimu zaidi.
“Baadhi ya wasimamizi wa mashine walikuwa hawana uelewa wa matumizi ya ‘Solar Panel’, kuna watu walikuwa wanaziweka chini ya miti na baadhi walikuwa wanazigeuza,” alisema Jaji Lubuva.
Akizungumzia kutofanikiwa kwa kazi hiyo, alisema idadi kubwa ya wananchi wasiojua kusoma na kuandika ilisababisha kazi ya utiaji alama na saini kuwa ngumu.
Alipoulizwa kuhusu hasara iliyopatikana wakati wa utekelezaji wa kazi hiyo, Jaji huyo mstaafu alisema bado haijajulikana kwa sababu bado hawajapokea taarifa kamili kutoka vituo vyote vilivyohusika katika uandikishaji.
Alisisitiza kuwa NEC imejipanga kuondoa kasoro zilizojitokeza katika mashine 7,750 zinazotarajia kuanza kutumika katika awamu ya kwanza ya uandikishaji na 250 zilizotumika katika majaribio zitafanyiwa marekebisho ili ziendane na hali ya hapa nchini.
Akitoa takwimu za watu waliohusika kwenye uandikishaji wa majaribio alisema Kata ya Bunju waliandikishwa 15,123, Mbweni 6,200 Mkoa wa Morogoro watu 19,188.
Alisema vitambulisho hivyo ndivyo vitakavyotumika katika upigaji wa kura ya maoni ya Katiba mpya mwezi Machi pamoja na Uchaguzi Mkuu Oktoba.
Zoezi hilo linatarajia kugharimu Sh bilioni 293 wakati hivi karibuni Jaji Lubuva alikaririwa na vyombo vya habari akikiri ofisi yake kupatiwa Sh bilioni 15 tu kwa ajili ya zoezi hilo.