Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
CHAMA cha Kutetea Haki za Walimu (CHAKAMWATA) kimemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Hapi, kuwaomba radhi walimu nchini au kuifuta kauli yake aliyoitoa Juni 16, mwaka huu.
Akiwa katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, DC Hapi alinukuliwa akisema: “Walimu wote wasioridhika na mshahara wao ni bora watafute shughuli nyingine ya kufanya”.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Chakamwata Mkoa wa Pwani, Mwalimu Abubakari Omary, alisema DC Hapi aliwatukana walimu kwa kauli yake hiyo.
“Mwalimu ndio msingi wa kutoa wataalamu nchini na wote mnajua umuhimu wake, hata Rais Dk. John Magufuli ni mwalimu, DC Hapi alitoa kauli hiyo ambayo tunaona kuwa alitutukana walimu.
“Nasema hivyo kwa sababu kimsingi tangu awamu ya tatu ya Rais mstaafu Benjamini Mkapa alipotangaza kufuta posho ya walimu, hadi leo kiasi cha mshahara anaoupata mwalimu hakiridhishi.
“Siwezi kusema ule ni mshahara bali ni posho, lakini bado walimu tumeendelea kufanya kazi ya kufundisha watoto kwa moyo, leo hii anakuja na kutoa kauli hii, tunamtaka aombe radhi au aifute kabisa,” alisema.
Alisema tayari wamemuandikia mkuu huyo wa wilaya barua yenye namba CMT.MWD/ WK/016/001 watakayoiwasilisha ofisini kwake ikifafanua suala hilo.
“Iwapo Serikali ina nia ya kuona kiwango cha elimu nchini kinainuka, tunaomba wasitusahau katika kutuboreshea maslahi yetu,” alisema.
Alisema chama chao ni kipya na kimesajiliwa kwa namba 031, Wizara ya Kazi na Ajira Machi 13, 2015 kikiwa na lengo la kutetea haki na maslahi ya walimu nchini.