NA LEONARD MANG’OHA (MSJ) DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Rasilimali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Hamad Rashid Mohamed, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama cha ADC.
Rashid aliteuliwa kushika wadhifa huo jana baada ya aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Said Miraji, kuvuliwa madaraka.
Uamuzi huo ulifikiwa jana katika mkutano mkuu wa chama hicho, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Akuzungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufanyika uamzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa wa ADC Taifa, Doyo Hassan Doyo, alisema katika mkutano wao walikubaliana pia kuwavua uongozi baadhi ya viongozi wao.
“Katika kikao chetu, tumekubaliana pia kuwavua uongozi na kuwavua uanachama baadhi ya viongozi ambao ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Taifa, Jumanne Magafu, Katibu Mkuu wa Chama chetu, Lydia Salanya na aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Ulinzi Taifa, Juma Wandwi,” alisema Doyo.
Kwa mujibu wa Doyo, kufukuzwa kwa wanachama hao, kunatokana na kukiuka taratibu mbalimbali za chama.
Alizitaja baadhi ya taratibu hizo, kuwa ni pamoja na kughushi nyaraka za chama na kuzungumza na vyombo vya habari bila ruhusa.