MMOJA wa marais wa zamani wa Burundi, Kanali Jean-Baptiste Bagaza, amefariki dunia mjini hapa jana akiwa na umri wa miaka 69.
Kanali Bagaza amekuwa akitibiwa kwa muda katika Hospitali ya Sainte Elisabeth ya hapa baada ya kuugua kwa muda mrefu.
“Imethibitishwa, Rais wa zamani Jean Baptiste Bagaza amefariki dunia akitibiwa Ubelgiji,” aliandika Mshauri wa Rais wa Burundi, Willy Nyamitwe kwenye Twitter.
Kauli kama hiyo pia iliandikwa katika mtandao huo na Rais Pierre Nkurunziza mwenyewe.
“Salamu za rambirambi kwa familia yake na Warundi wote,” alisema Rais Nkurunziza.
Kanali Bagaza aliyezaliwa Agosti 29, 1946 aliingia madarakani Novemba 1976 kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi akianzia uenyekiti wa Baraza Kuu la Mapinduzi Burundi na baadaye rais.
Hata hivyo, naye aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi mengine yaliyoongozwa na binamu yake, Meja Pierre Buyoya Septemba 1987.
Alipinduliwa akiwa nje ya nchi yake na hivyo alienda kuishi uhamishoni Uganda na baadaye Libya hadi mwaka 1993 aliporudi nyumbani.
Tangu mwaka 1994 amekiongoza Chama cha Ufufuko wa Taifa (PARENA) na kutokana na hadhi yake kama mkuu wa zamani wa nchi, amefariki dunia akiwa seneta wa maisha.
Anakumbukwa kwa kujenga sehemu kubwa ya miundombinu iliyopo sasa nchini humo wakati wa utawala wake ambao ulikuwa moja ya vipindi ambavyo kulikuwa na udhabiti wa kisiasa katika historia ya taifa hilo baada ya uhuru.