KWENYE makala moja iliyobeba kichwa cha habari “Kwa ukwapuaji hautofautiani na Nigeria” kwenye Gazeti hili Januari 27 mwaka huu, nilifahamisha namna ambavyo maofisa waandamizi wa Serikali ya nchi hiyo walivyokuwa wamekwapua mabilioni ya fedha kutoka kwenye mabenki ya nchi hiyo.
Hali hiyo haikutofautiana na hali ya ukwepaji kodi uliofanywa na baadhi ya watu kwenye Serikali nchini Tanzania na jinsi walivyokwapua mabilioni ya fedha kutoka Benki Kuu mambo yaliyoibua kashfa kadhaa na hata kusababisha baadhi ya maofisa hao kujiuzulu.
Wakati nchini Nigeria unaweza kusikia kuwa lori la mafuta limeibwa na lisionekana licha ya kwamba lilipita kwenye barabara ndani ya miji ya nchi hiyo kwa Tanzania unaweza kusikia kontena lilipita kwenye Bandari ya Dar es Salaam kimya kimya na si mtoza kodi wala ushuru aliyeliona.
Pamoja na hali hiyo suala jingine ambalo linaonesha kuwa kila linalotokea Nigeria mwangwi wake hupokelewa na Tanzania ni hili kadhia ya kuwapo kwa wafanyakazi hewa kwenye ofisi za umma na hivyo kuifanya Serikali kupoteza fedha nyingi. Hivyo Taasisi ya Kupambana na Rushwa nchini Nigeria imebaini kuwapo kwa wafanyakazi hewa 37,000 kwenye orodha ya malipo ya wafanyakazi serikalini na kwamba idadi hiyo bado itaongezeka.
Kaimu mwenyekiti wa Taasisi hiyo inayojulikana kama Tume ya Uchumi na Uhalifu wa Kifedha (EFCC), Ibrahim Magu alisema kuwa maelfu ya wafanyakazi ambao hawapo kwenye orodha ya wafanyakazi serikalini imeigharimu Serikali takribani fedha za Nigeria Naira bilioni 1 ambazo ni sawa na Dola za Marekani milioni 5.
Magu akizungumza kwenye tukio la kupambana na rushwa katika wizara ya Serikali jijini Abuja alisema, “Idadi hiyo itaongezeka kwani tunataka kufukua wafanyakazi hewa waliojificha ndani kwenye orodha ya malipo ya watumishi wa umma katika majimbo.”
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari alizindua mapambano dhidi ya rushwa serikalini tangu alipoapishwa Mei 2015. Wizara ya Fedha, Februari mwaka huu ilisema kuwa iliondoa wafanyakazi hewa wengine 24,000 kutoka kwenye orodha nyingine ya malipo serikalini ambapo kwa mwezi huo iliokoa fedha za Nigeria Naira bilioni 2.29 sawa na Dola za Marekani milioni 11.5. Magu alibainisha kuenea kwa udanganyifu unaofanywa kwenye manunuzi ndani ya wizara za Serikali na kwenye huduma za umma na kuonya watakaokiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Nigeria watakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 10 jela.
Alibainisha kuwa tume imeanzisha kitengo maalumu cha kushughulikia masuala ya udanganyifu kwenye manunuzi na kikiwa kama wakala wa Serikali kimekuwa kinapokea mashtaka kadhaa kuhusu suala hilo. Alisema tume hiyo imedhamiria kwa kina kuliko ilivyokuwa awali kuondoa shughuli zote za udanganyifu kwenye wizara, idara na mashirika ya umma.
Mapambano dhidi ya rushwa yaliyoanzishwa na Buhari yameshasababisha kukamatwa kwa watu wenye nafasi za juu serikalini kuhusiana na manunuzi ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 2.1 kashfa ambayo ilitokea kwa kununua silaha katika jitihada za Serikali za kupambana na Boko Haram.
Waliokamatwa kuhusiana na kashfa hiyo ni pamoja na Mshauri wa zamani wa Usalama wa Taifa, Sambo Dasuki na Msaidizi wa Rais wa zamani, Goodluck Jonathan, Waripamowei Dudafa, ambaye anatuhumiwa kupokea sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kutumika kwenye kampeni za awali za urais kwenye chama cha PDP Desemba 2014.
Licha ya kuanzishwa kwa mapambano hayo dhidi ya rushwa ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Transparency International ilibainisha kuwa asilimia 75 ya raia wa Nigeria wanaamini kwamba rushwa ndani ya Serikali ilikuwa imeongezeka katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Ukaguzi uliofanywa kwenye akaunti za wafanyakazi kwa kutumia takwimu za kibaiometriki kuthibitisha idadi na kufanya utambuzi wa wamiliki wa akaunti kwenye mabenki ambako hutumiwa na Serikali kulipia mishahara ya wafanyakazi wake, uligundua watumishi wengi waliokuwa wakipokea mishahara majina yao hayaendani na majina yaliyopo kwenye akaunti na baadhi walikuwa wakipokea mishahara kutoka vyanzo tofauti.
Hata hivyo Mshauri Maalumu wa Waziri wa Fedha, Festus Akanbi alisema kwamba wizara hiyo imeshafanya ukaguzi wa wafanyakazi 312,000 na kwamba itakuwa inaendeleza kazi hiyo kwa kutumia mbinu saidizi za ukaguzi kwa kutumia kompyuta katika mapambano yake dhidi ya rushwa nchini humo.
Rushwa imekuwa ni tatizo kubwa nchini Nigeria tume imeshakamata Dola za Marekani trilioni 2 zilizoibwa kutoka kwenye fedha za umma tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003
tangu Buhari alipotangaza mapambano dhidi ya rushwa baadhi ya nakala zinazohusu Bajeti ya mwaka huu zimetoweka kutoka kwenye Bunge na ukiukwaji mkubwa wa kanuni kama vile kubainika kwa Naira milioni 795 sawa na Dola za Marekani milioni 4 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuboresha wavuti wa wizara moja kumesababisha ‘kutumbuliwa jipu’ kwa Mkuu wa Ofisi ya Bajeti na hivyo kucheleweshwa kuthibitishwa kwa mpango wa fedha kwa mwaka 2016.
Katika hili suala la wafanyakazi hewa Tanzania haiwezi kujitofautisha na Nigeria na ni dhihirisho kuwa kila aina ya kadhia ya kifisadi inayofanyika hapa ni sawa na kudurufu kadhia ambayo ilishafanyika huko Afrika Magharibi.
Suala la wafanyakazi hewa limekuwa ni kama kikaango cha watendaji wa Serikali ya Magufuli kwani wasipolitekeleza kwa makini huwa inakula kwao, kwani hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela pamoja na Katibu Tawala wa mkoa huo, Abdul Dachi walitumbuliwa jipu baada ya kudai kuwa mkoani humo hakuna wafanyakazi hewa. Awali ripoti iliyotolewa baada ya ukaguzi wa wafanyakazi hewa nchini ilibaini kuwa Serikali imekuwa ikiwalipa wafanyakazi hewa takriban 2,000 kutoka mikoa mbali mbali na kwamba Serikali imekuwa inapoteza mamilioni ya dola kwa ubadhirifu huo.
Rais wa Tanzania, John Magufuli alitoa siku 15 kwa wakuu wa idara na taasisi mbalimbali za Serikali kufanya ukaguzi na kuwaondoa wafanyakazi hewa serikalini. Rais Magufuli ambaye aliingia madarakani miezi saba baada ya Buhari wa Nigeria kuwa madarakani amejikuta akiwa na changamoto zinazofanana na zile anazokabiliana nazo kiongozi huyo wa Nigeria.
Wafanyakazi hewa waliobainika nchini ambao ni takribani 2,500 wamekuwa wakipokea mshahara unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani milioni 1.0 kila mwezi.
Hata hivyo baada ya agizo la Rais Magufuli la kusakwa kwa watumishi hao hewa hivi sasa inakadiriwa kuwa wafanyakazi hao hewa wanakadiriwa kufikia 6,000. nRushwa, ubadhirifu wa fedha za umma pamoja na vitendo vya ufisadi unaonekana kuwa ni moja ya mambo ambayo alisema kuwa yamesababisha baadhi ya watu wachache kujiona kuwa wamo peponi huku wengine wakitopea kwenye lindi la ufukara wakiteseka.