24.5 C
Dar es Salaam
Friday, September 27, 2024

Contact us: [email protected]

Atakayepiga ‘hole in one’ kuondoka na ndinga NMB CDF Trophy

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Mashindano ya gofu ya Kombe la Mkuu wa Majeshi ‘NMB CDF Trophy’ yanatarajiwa kufanyika Oktoba 4-6,2024, huku mchezaji atakayefanikiwa kupiga ‘hole in one’ atapewa zawadi ya gari aina ya Toyota Harrier yenye thamani ya sh milioni 70 na kwenda kupumzika hoteli ya Serena .

Gari hiyo imekabidhiwa leo Septemba 27,2024 na Meneja Mkuu wa Toyota kwa kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, jijini Dar es Salaam, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo.

Akizungumzia mashindano hayo yatakayofanyika katika viwanja vya klabu Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Luwongo amesema mchezaji atayepiga ‘hole in one’ atakabidhiwa gari yake muda huo huo na italipiwa kila kitu.

Ameeleza lengo mashindano kuwa ni kumuenzi mlezi wa klabu ambaye ni Mkuu wa Majeshi ambapo kwa sasa ni Jenerali Jacob Mkunda na siku ya kufunga ndiye atakuwa mgeni rasmi.

Amesema kuwa pamoja kumuenzi Mkuu wa Majeshi lakini pia ni muendelezo wa sherehe za kuzaliwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambayo kila mwaka huadhimishwa Septemba Mosi.

“Niseme kuwa ni shindano kubwa, ni shindano ambalo kila siku mlezi anapenda kuliboresha ili kuwa shindano kubwa kuliko mashindano yote ya gofu yanayofanyika nchini,” ameeleza.

Amesema maandalizi mashindano hayo ambayo mdhamini mkuu ni benki ya NMB yamekuwa bora zaidi huku zawadi zikiboreshwa, washindi watapata fedha tasilumu ambapo mshindi wa jumla atapata Sh milioni 4.

“Safari hii aina ya zawadi ambazo tumezianda ni za kipekee na kubwa,tumebadilisha mtindo wa aina ya zawadi, badala kumpa mshindi TV au friji, safari hii tutatoa fedha tasilimu zilizotoka kwa mdhamini mkuu ambaye ni NMB,” amefafanua.

Naye Mkuu wa Idara ya Wateja Maalum wa benki ya NMB, Getrude Mallya ambaye alikabidhi hundi ya sh milioni 35 za udhamini wa mashindano hayo amesema wamekuwa wakishirikiana na Klabu ya Gofu Lugalo kwa kipindi cha miaka saba sasa.

Amesema lengo la kuendelea kutoa udhamini huo ni kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa weledi na ubora.

“Mashindano haya yamekuwa yakifanyika kila mwaka na benki yetu imeendelea kushirikiana na kutoa udhamini wa Kombe hili la Mkuu wa Majeshi hadi sasa tumetoa kiasi cha fedha kisichopungua milioni 200 kufanikisha mashindano haya,” amesema Getrude.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa kampuni ya Toyota, Kadiva William, amesema tofauti na gari waliyotoa, imeandaa sehemu ambayo wachezaji watakuwa wanafanyiwa ‘massage’ katika kipindi chote cha mashindano.

Aidha Nahodha wa Klabu ya Gofu Lugalo, Meja Japhet Masai amesema mashindano hayo yatashirikisha wachezaji wakulipwa na ridhaa kwa vipengele vyote pamoja na watoto.

Ameeleza kuwa mchezaji atakayefanikiwa kupiga ‘hole in one’ ambayo atatakiwa kupiga mpira umbali wa mita 75 na kuingia moja kwa moja shimoni, itakuwa amevunja rekodi kwani kwa muda mrefu hakuna aliyewahi kufanya hivyo katika mashindano licha ya kuwa wanapiga wakati wa mazoezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles