Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema hali ya uzalishaji wa umeme ni inaendelea kuimarika ambapo kufikia leo Oktoba 2, 2023 upungufu wa umeme ni Megawati 300 hadi 350.
Judith amesema hayo leo wakati alipotembelea kituo cha uzalishaji wa umeme wa gesi asilia megawati 43 cha Tegeta, Dar es Salaam kuwa mitambo minne inafanya kazi na mmoja upo katika matengenezo na utakamirika hivi karibuni.
Amesema wiki iliyopopita alisikia kwenye taarifa kuwa gridi la Taifa kuna upungufu wa umeme wa Megawati 400.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa kutokana na uzalishaji kwa siku mahitaji yakiwa juu uzalishaji ukiwa mdogo upungufu unakuwa mkubwa lakini uzalishaji ukiwa mkubwa mahitaji yatakuwa madogo na kituo cha Ubungo namba 1 na 2 uzalishaji unaendelea kama kawaida.
Amesema kikubwa ambacho amewaelekeza TANESCO ni kuhakikisha matengenezo ya mitambo yafanyike kwa wakati na muda mfupi ili kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme.
“Hii ni kuhakikisha inapotokea hitirafu zinafanyiwa kazi kwa haraka ili umeme uendelee kupatikana lakini pamoja na kuja kukagua kituo nimewaelekeza TANESCO kuendelea kuhimarisha huduma kwa wateja,” amesema.
Amesema watanzania wanapopata changamoto za umeme na hitirafu za luku majumbani au umeme umekata au waya na transforma ina shida wahakikishe wanatatua changamoto hizo kwa wakati kuepuka wananchi kulala giza .
Akizungumzia uunganishaji wa umeme katika maeneo ambayo tayari ina miundombinu, Judith amewataka TANESCO kuhakikisha wanaweka mfumo wakupunguza mianya ya rushwa.
“Changamoto zinaendelea kutokea katika suala zima la kuunganisha umeme, kwa kweli kitu hiki kinaendelea kutuumiza sana kwa hiyo TANESCO wahakikishe sehemu ambayo kuna miundombinu na wananchi wameomba umeme waunganishiwe kwa wakati ili kila mmoja afurahie huduma ya umeme,” amesema.
Ameonya kuwa suala kukata umeme masaa 12 haitokubalika na kuwataka wakae pamoja kwenye maofisi ya Serikali na kukubaliana njia sahihi ya kukata na kurudisha.
“Kama unafanya kazi saa moja hadi saa 12 wakae wakubaliane mfumo ambao ni sahihi labda saa nane hadi saa 4 usiku ili shughuli za uzalishaji ziweze kuendelee,”amesema.
Amefafanua kuwa mitambo ya gesi ina changamoto zake, hivyo TANESCO kwa kushirikiana na TPDC wanaweka mpango kwenye vyanzo vya gesi kuweza kuhakikisha wanapata gesi nyingi zaidi.
Amesema kama nchi lazima wawe na vyanzo tofauti vya umeme ili uwe unapatikana kwa hali ya watanzania na waweze kumudu bei yake kutokana na uwepo wa vyanzo vingi.Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amesema kwa sasa shirika hilo kwa kushirikiana Wizara ya Nishati wanafanya juhudi zinazowezekana kuhakikisha wanakuwa na umeme wa kutosha kwenye gridi kuwawezesha kugawa kwa wananchi kwa shughuli za kawaida.