30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Msanii  Beatrice Mashala aandaa onesho la sanaa ya uchoraji Dar

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Msanii chipukizi katika tasnia ya sanaa ya uchoraji nchini, Beatrice Mashala, ameandaa onesho la kazi zake litakayofanyika katika ukumbi wa The Drum uliopo Masaki jijini Dar es Salaam kuanzia Jumamosi ya Septemba 2, yatakapofunguliwa rasmi hadi Septemba 30, mwaka huu.

Msanii Beatrice Mashala akiwa kazini.

Akiongea katika mahojiano maalum kuhusiana na onesho hilo, Beatrice alisema kuwa onesho hilo ameliandaa kwa ajili ya kutangaza kazi zake zake za sanaa ya uchoraji na hili ni onyesho lake la kwanza japo amekuwa  akishiriki katika maonesho mbalimbali ya tasnia hiyo nchini pia amekuwa na kituo cha kutangaza na kuuza picha zake mjini Arusha.

”Tangu nianze kujihusisha na sanaa ya uchoraji mnamo mwaka 2020 nimekuwa nikishiriki maonesho yaliyoandaliwa na wasanii wenzangu na kazi zangu zimekuwa zikivutia watu wengi,” amesema Beatrice.

Alisema ameweza kuchora picha za sanaa na za watu binafsi ambazo zimekuwa zikivutia watu wengi pia amechora picha za viongozi  mbalimbali ambazo pia zitakuwepo katika maonesho haya ya kazi zake.

Akizungumzia tasnia ya sanaa ya uchoraji nchini, Beatrice ambaye kitaaluma ni Mwanasheria mwenye shahada ya kwanza ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Makumira kilichopo mkoani Arusha, alisema hapa nchini kuna wasanii wenye vipaji vikubwa katika tasnia ya uchoraji na wenye taalauma hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam japokuwa tasnia hiyo imekuwa haipati kipaumbele kikubwa katika kuikuza na kuiendeleza kama zilivyo sanaa nyingine.

 “Kama ilivyo kwenye tasnia ya michezo kwenye sanaa pia kuna sanaa za aina nyingi na wasanii wa fani mbalimbali ila unakuta baadhi ya sanaa zinapewa kipaumbele zaidi na zina washabiki na wapenzi wengi wakati kuna baadhi ya sanaa bado zina mwamko mdogo na wafuasia wake ni wachache,” amesema.

Msanii Beatrice Mashala akionyesha kazi zake katika moja ya maonesho ya sanaa aliyoshiriki mjini Arusha hivi karibuni.

Beatrice alisema uchoraji wa picha unaweza kuwa kipaji au ujuzi ambao mtu anajifunza kwa ajili ya kujipatia kipato, kujifurahisha na kuwapatia wengine kama zawadi ili kudumisha upendo kwenye jamii. Picha zinazongumziwa hapa ni zile zinazochorwa kwa kalamu kwenye karatasi au sehemu maalum ambayo itabeba ujumbe fulani kwa mtu au jamii.

Aliongeza kusema kuwa kama zilivyo kazi nyingine halali, uchoraji pia ni kazi halali ambayo mtu akiwekeza muda na rasilimali ana uhakika wa kupata kipato kumuwezesha mtu kupata mahitaji ya msingi:

“Kuifanya sanaa ya uchoraji unahitaji eneo la kufanyia kazi, malighafi ikiwemo brashi za kucholea, kanvasi na rangi kwa ajili ya kutekeleza kazi zako pia ni moja ya kazi ambayo haitumii mtaji mkubwa kuifanya,”alisema Beatrice.

Alitoa wito kwa wasanii wenzake kutokata tamaa badala yake wazidi kupambana kufanya kazi nzuri na kuzitangaza kwa nguvu zote, na aliomba Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni na taasisi za kusimamia utamaduni kufanya kazi kwa karibu na wasanii kwa kuwaongoza na kuwaonyesha fursa mbalimbali zilizopo katika tasnia hii.

“Michezo,Sanaa naUtamaduni ni moja sekta ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kutoa fursakwa vijana wengi wa Tanzania kujiajiri na kujikwamua kimaisha,” alisema.

Kuhusu wasanii wanaomvutia katika tasnia ya uchoraji alisema wapo wengi ila msanii Sungi Mlengeya anamvutia zaidi na anatamani kupata mafanikio yaliyofikiwa na msanii huyo ambaye amefikia hatua ya kuwa na gallery ya kusimamia kazi zake.

Pia, alimtaja Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Elias Jengo, kuwa ni hazina kubwa kwa Taifa ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwafundisha na kuwaongoza wasanii wengi chipukizi katika sanaa za aina mbalimbali.

 Kuhusiana na matarajio yake ya baadaye, Beatrice Mashala,alisema kuwa ni kufanya kazi kwa bidiii hadi kufikia hadhi ya kuwa msanii wa kimataifa pia ana ndoto za kujiendeleza kusomea fani hiyo ili kupata ujuzi zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles