Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amewataka wananchi wanaopewa hati miliki za ardhi kuacha mara moja tabia ya kuuza ardhi zao kwa watu wengine kiholela badala yake waziendeleze kwa ajili yao na vizazi vijavyo.
Pinda ameyasema hayo wakati akikabidhi hati miliki za kimila kwa baadhi ya wakazi wa kijiji cha vikonge Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ikiwa ni moja ya njia kuwawezesha wananchi kiuchumi, kusaidia katika kutatua migogoro ya ardhi na kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Pinda pia amewasisitiza wananchi waliopewa hati kuwa watumie hati hizo katika kujiendeleza kiuchumi kwa kutumia kama dhamana katika mabenki mbalimbali hapa nchini na kuendeleza ardhi zao au katika shughuli nyingine za kiuchumi.
Aidha, Pinda amewataka viongozi wa vijiji kuacha mara moja tabia ya kuuza kiholela maeneo ya umma na badala yake kuyatunza kwa ajilli ya huduma za kijamii kama vile Afya, Shule, misitu na hifadhi.