25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

93,019 KUJIUNGA KIDATO CHA TANO, 2,999 WAKOSA NAFASI

NA RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

JUMLA ya wanafunzi 2,999 wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alipokuwa akitoa taarifa ya uchaguzi na upangaji wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka huu.

Simbachawene alisema kati ya wanafunzi 96,018, ni wanafunzi 93,019 ndio wenye sifa za kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi, kwa kuwa wamefaulu vigezo vilivyoainishwa.

Alisema kati ya hao, wanafunzi 92,998 ni wa shule (school candidates) na 21 walisoma chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Pia alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwa mwaka huu wanatoka kwenye shule za Serikali na zisizokuwa za Serikali, huku shule 351 zikiwamo 17 mpya zimepangiwa wanafunzi hao.

Alisema mwanafunzi atakayechelewa kuripoti shuleni ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya kufungua shule nafasi yake itachukuliwa na mtu mwingine.

“Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano kwa mwaka 2017 unaanza Julai 17, mwaka huu, lakini kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha sita wao watafungua  Julai 3, mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa,” alisema na kuongeza:

“Kwa kuwa upangaji wa wanafunzi wanaoingia kidato cha tano kwa mwaka 2017 umezingatia machaguo ya wanafunzi  wenyewe na nafasi zilizopo katika shule husika, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule.

“Nitumie nafasi hii kuwaagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati na endapo mwanafuzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya kufungua shule, nafasi yake itachukuliwa na mtu mwingine.’’

Alisema jumla ya watahiniwa wa shule 349,524, wakiwamo wasichana 178,775, sawa na asilimia 51.1 na wavulana 170,749 sawa na asilimia 48.9 walifanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka jana.

Simbachawene alisema watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo mwaka jana walikuwa 47,751, wakiwamo wasichana 24,587, sawa na asilimia 51.5 na wavulana 23,164, sawa na asilimia 48.5.

Simbachawene alisema watahiniwa waliofaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu ni 96,018, sawa na asilimia 27.60 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo kwa Tanzania Bara.

“Hivyo ufaulu katika mwaka 2016 uliongezeka kwa asilimia 3.15 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2015,’’ alisema.

Alitoa ufafanuzi kuhusiana na taratibu walizozitumia kuwachagua kuwa walitumia mwongozo wa uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano.

Alisema mwongozo huo unamtaka mwanafunzi anayeomba kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari na vyuo vya ufundi kujaza fomu ya uchaguzi.

“Hiyo ndiyo fomu rasmi ya maombi ya kuchaguliwa, hivyo kwa kutumia fomu hiyo, mwanafunzi hujaza machaguo matano ya tahasusi (combination) za masomo anayotaka kusoma na shule anayoipenda kujiunga nayo kwa kila chaguo,’’ alisema.

Simbachawene alisema uchaguzi na upangaji huo umezingatia mwongozo wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi wa Mei 15, mwaka huu.

Alisema mwongozo huo unaelekeza kwamba kigezo cha mwanafunzi kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi ni kupata alama AAA hadi CCD katika masomo ya tahasusi.

Alisema kigezo kingine ni kupata alama tatu na pointi zisizopungua 25 katika daraja, machaguo yaliyojazwa na mwanafunzi katika fomu ya kuchagua na nafasi zilizopo katika shule husika.

“Napenda kusisitiza kuwa, vigezo hivi ndivyo vilivyotumika kwa wanafunzi kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka huu, nia ni kuinua kiwango cha ujuzi kwa elimu ya juu nchini,’’ alisema.

Pia aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha shule zilizopelekewa fedha za kuongeza miundombinu ya kidato cha tano kupitia mpango wa elimu bila malipo kulingana na matokeo wahakikishe ujenzi unakamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles