24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

91,108 waomba ajira, Serikali yatoa kibali waajiriwe 4,549

Na AZIZA MASOUD

DAR ES SALAAM 

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imepata kibali cha kuajiri walimu 4,549 kwa shule za msingi na sekondari.

Walimu hao ni miongoni mwa waombaji 43,770 waliobainika kuwa na vigezo ambao ni sawa na asilimia 48.04 ya waombaji wote 91,108 waliowasilisha maombi yao.

Akizungumza jana, Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, alisema waombaji 91,108 walijitokeza kutuma maombi ya nafasi mbalimbali za ualimu zilizotangazwa na ofisi hiyo.

Alisema kati ya hao, 43,770 sawa na asilimia 48.04 ya waombaji wote walikuwa na viambatanisho vyote vilivyohitajika wakati 47,338 sawa na asilimia 51.96 maombi yao hayakuwa na vigezo.

“Kati ya waombaji  43,770 wenye vigezo, wizara imepata kibali cha kuajiri walimu 4,549. Kati ya walimu hao, walimu 3,059 sawa na asilimia 67.25 wamepangwa kufundisha shule za msingi wakati walimu 1,490 sawa na asilimia 32.75 wamepangwa kufundisha sekondari,” alisema Jafo.

Alisema kutokana na mahitaji makubwa ya walimu katika shule za msingi na sekondari kwa masomo ya sayansi, wizara imefanya uchambuzi na kutoa vipaumbele katika ajira za walimu daraja la tatu A (wenye cheti) kwa ajili ya kufundisha shule za msingi.

“Walimu wa daraja la tatu B (wenye stashahada) wa masomo ya sayansi wamechukuliwa kwa ajili ya kufundisha shule ya sekondari kidato cha kwanza hadi nne na walimu daraja la tatu C  shahada wa masomo ya sayansi, kwa ajili ya kufundisha kidato cha tano na sita,” alisema.

Alisema walimu daraja la tatu C, shahada wa masomo ya elimu maalumu, biashara, uchumi, kilimo na maarifa ya nyumbani, wamechukuliwa kufundisha shule ya sekondari.

“Mchakato wa kupitia maombi ulijumuisha uhakiki wa uhalali wa vyeti vya elimu ya taaluma vya waombaji na ukamilishaji wa nyaraka zilizohitajika,” alisema Jafo.

Alisema kwa waombaji  wa masomo ya sayansi na sanaa ambao walitimiza vigezo lakini hawakufanikiwa kupata nafasi kwa kipindi hiki, maombi yao yalichambuliwa na yamehifadhiwa katika kanzidata ya Tamisemi ili waweze kupewa kipaumbele wakati ujao.

Aidha Jafo ametoa angalizo kwa wazazi ambao wanapeleka vimemo vya maombi kwa wakurugenzi wa halmashauri, ambavyo vinawaombea watoto wao kupata kazi maeneo ya mijini na kuacha shule za vijijini zikiwa hazina walimu.

“Wazazi ambao wanasambaza vimemo kwa wakurugenzi kutaka watu wakae katikati ya halmashauri hatutawabadili, mkurugenzi hatakiwi kubadilisha mtu bila kibali kutoka kwa Katibu Mkuu wa Tamisemi, tumepanga walimu kulingana na mahitaji,” alisema Jafo.

Akizungumzia kuhusu wingi wa waombaji wa nafasi hizo, Jafo alisema inatokana na walimu wengi wa shule za binafsi kutamani kufanya kazi katika shule za Serikali.

“Kwa sasa waombaji wamekuwa wengi kwa sababu walimu wengi waliokuwa katika sekta binafsi wametamani kuingia serikalini, wapo pia waliowahi kufundisha serikalini zamani wakaacha, lakini kwa sasa wanataka kurudi tena serikalini baada ya kuona kazi nzuri inayofanywa na Serikali katika kuwahudumia walimu,” alisema Jafo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles