22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Mkakati madhubuti utaimarisha sekta ya uvuvi

TANZANIA ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili.

Rasilimali hizo ni pamoja na sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki ambazo ni muhimu katika kubadili uchumi wa nchi ikiwa hatua zaidi zitachukuliwa ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na uvuvi haramu kwa bahari na maziwa makuu nchini hasa kwa jamii zinazoishi jirani na ukanda huo.

Ni wazi kwamba katika kuelekea uchumi wa kati wa viwanda, Rais Dk. John Magufuli amekuwa akisisitiza kila mara kuwa kama nchi itatumia vizuri rasilimali zake, itafika wakati itakuwa na uwezo wa kutoa misaada kwa nchi nyingine badala ya kutegemea misaada kutoka mataifa mengine kama ilivyo sasa.

Takwimu zinaonesha kuwa nchi yetu imejaliwa maeneo mengi ya maji ambayo ni muhimu katika shughuli za uvuvi ambazo huwapatia wananchi lishe, kipato na ajira.

Maeneo hayo hujumuisha eneo la maji baridi na maji bahari. Eneo la maji baridi hujumuisha maziwa makuu matatu ambayo ni Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.

Aidha, kuna maziwa ya kati na madogo 45, mito 29, mabwawa ya asili na ya kuchimbwa pamoja na maeneo oevu.

Kwa upande wa maji ya bahari, Tanzania ina ukanda wa pwani wa Bahari ya Hindi wenye urefu wa kilometa 1,424.

Katika maeneo haya kuna rasilimali nyingi za uvuvi ambamo shughuli za uvuvi hufanyika.

Taarifa za utafiti zilizofanyika kwa vipindi tofauti zinaonesha kwamba, kiasi cha samaki kilichopo katika maziwa makubwa ni takriban tani 2,914,296 huku Ziwa Victoria likiwa na tani 2,451,296, Ziwa Tanganyika tani 295,000 na Ziwa Nyasa tani 168,000.

Kutokana na umuhimu wa sekta ya uvuvi, sasa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Norway (Norad), imesaini mkataba wa uzalishaji samaki aina ya sato tani 100,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Katibu Mkuu Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Rashid Tamatamah, anasema kwamba mradi huo umekuja muda mwafaka wakati nchi ina mahitaji makubwa.

Tunajua lengo la Serikali ni kuzalisha samaki kwa wingi ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kwenye mabwawa.

Katika kipindi cha miaka 20 sasa Tanzania imekuwa haifanyi vizuri katika sekta ya uvuvi ambapo imekuwa ikizalisha samaki tani 350,000 hadi 380,000 kwa mwaka.

Hata hivyo kulingana na taarifa rasmi za Serikali inaonesha kwamba samaki wanaozalishwa hivi sasa kwenye vyanzo vya maji idadi yake imebaki kuwa vilevile, haiongezeki kwa kasi hivyo kuna kila haja ya kuongeza kasi ya uzalishaji.

Kuanzishwa kwa mradi huo ambao utatekelezwa Kibaha mkoani Pwani kutawafanya vijana wengi kutapata fursa ya elimu pamoja na kuzalisha samaki.

Sisi MTANZANIA tunapongeza hatua hiyo ya Serikali kwa kushirikiana na Norway kama njia madhubuti ya kuimarisha sekta ya uvuvi nchini.

Hivyo tunaishauri Serikali kuhakikisha inaweka nguvu ili mradi huo uweze kutekelezwa na ni wazi utasaidia kuimarisha uchumi wa nchi yetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,057FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles