25.4 C
Dar es Salaam
Thursday, January 20, 2022

Serikali yashtukia ‘dili’ watoto kukatisha masomo

Na SARAH MOSES-DODOMA

OFISA Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Chamwino mkoani hapa, Sophia Swai amesema wamebaini mbinu mpya ya wazazi kuwakatisha watoto wao wa kike masomo ili wakafanye kazi za ndani.

Mbali na hayo, alisema pia kumekuwapo na changamoto kubwa wilayani humo ambayo wazazi hutaka watoto wao hasa wa kike waandike ‘madudu’ kwenye mitihani ili wasifaulu na wabaki nyumbani kwa lengo la kuwaoza au kuwapeleka mijini kwenda kufanya kazi za ndani.

Sophia aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa watendaji wa kata na vijiji ulioandaliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Woman Wake Up (WOWAP) linalotekeleza mradi wa kutokomeza ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni.

“Tumegundua mbinu mpya wanayotumia wazazi,  wamekuwa wakikataza watoto wao kwenda shuleni ili baada ya miezi mitatu waonekane ni watoro wa kudumu na kisha kufutwa shule.

“Katika Kijiji cha Manchali kilichopo Wilaya ya Chamwino, wazazi walifanya makusudi ili mtoto wao asifike shuleni kwa siku 90, na kusababisha mtoto akafutwa shule kisha wakampeleka Dar es Salaam kufanya kazi za ndani,” alisema. 

Aidha Sophia alisema kuanzia sasa wataanza kuwafuatilia watoto wote watoro na kama wazazi wanahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Mpwayungu, Peter Chugu alisema wazazi bado wanaendelea kuwaozesha watoto wa kike wakiwa katika umri mdogo.

“Katika tukio la hivi karibuni wanafunzi wawili wa kidato cha tatu na nne walipata ujauzito, lakini walikataa kuwataja wahusika, hivyo hali kama hii imekuwa ikisababisha wahusika kutojulikana na kuendelea kuharibu maisha ya watoto wa kike,” alisema Chungu. 

Hata hivyo, Mratibu wa WOWAP, Nasra Suleiman alisema wataendelea kushirikiana na watendaji hao ili kubaini vitendo vyote vya ukatili vinavyoendelea katika jamii sambamba na kuibua matukio ya mimba na ndoa za utotoni.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,434FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles