29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Mkuu wa Majeshi awapa neno vingozi wa dini

Na MWANDISHI WETU-SIMIYU

MKUU wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuendelea kuhubiri amani ili kujenga jamii iliyo bora yenye kudumisha upendo na mshikamano.

Jenerali Mabeyo alitoa wito huo wakati wa ibada ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro, Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dk. Benard Kibese na viongozi wengine wa chama na Serikali.

Jenerali Mabeyo alisema kuwa amani ni msingi wa maendeleo kwa taifa lolote duniani.

“Suala la amani na utulivu ni la msingi sana katika nchi yetu, kwa vile kila mwananchi ana dini yake tunaamini kuwa viongozi wa dini zote kwa kuwa wanasikilizwa sana na waumini  wakiweka msisitizo katika suala la amani, amani itatawala na kutakuwa na utulivu.

“Utulivu huu tunauhitaji sana ili tupate maendeleo,  kama  viongozi wetu wa kisiasa wanavyosisitiza kuwa tudumishe amani na utulivu  tupate maendeleo, bila utulivu watu wakiwa wanahaingaika hakuna maendeleo kwa sababu hakuna shughuli mtu anaweza kufanya kama hana amani na utulivu, hivyo hataweza pia kuleta maendeleo yake, familia, jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Jenerali Mabeyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro, alisema vitendo vingi vya uvunjifu wa amani na uhalifu ikiwemo ukataji wa mapanga na mauaji ya vikongwe vinachangiwa na watu kukosa hofu ya Mungu.

Alisema hivyo nyumba za ibada zinapojengwa kwa wingi zitakuwa msaada mkubwa sana kwa watu kuwa na hofu ya Mungu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema jamii inayoamini uwepo wa Mungu haiwezi kuwa na vitendo vya kisasi, kukatana mapanga na mauaji ya vikongwe huku akiwaasa Watanzania kukaa kwa amani na upendo bila kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha amani.

Akibariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro, Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega, Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu aliwataka Watanzania kupendana na kuacha roho ya ubinafsi na visasi.

“Palipo na msamaha pana umoja, uelewano na usawa, lakini palipo na kisasi hapana maendeleo; nyumba ya ibada isitumike kama jukwaa la wanasiasa,” alisisitiza Askofu Sangu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles