450 WA VYETI FEKI WARUDISHWA KAZINI

0
1088

NA TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


WATUMISHI wa umma 450 walioondolewa kazini kutokana na kudaiwa kutumia vyeti vya kughushi wamerudishwa kazini baada ya kushinda rufaa zao.

Mbali na hilo, Serikali imesitisha mishahara kwa watumishi wa umma ambao walitakiwa kuwasilisha vyeti vyao kwa uhakiki lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk.Laurean Ndumbalo alisema watumishi hao wameshinda rufaa zao hivyo wataandikiwa barua za kurudishwa katika utumishi wa umma.

Alisema katika rufaa hizo, wengi walikuwa wanawake walioolewa na kubadili majina yao kwa kutumia ya waume zao.

“Kuna baadhi walitumia majina mawili alipokuwa kidato cha nne baadaye alilazimika kutumia matatu na kusababisha mkanganyiko hivyo tumejiridhisha na wanarudishwa katika utumishi wa umma,” alisema Dk. Ndumbalo.

Alisema Serikali pia imesitisha mishahara kwa watumishi wa umma ambao walitakiwa kuwasilisha vyeti vyao kwa uhakiki lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo.

“Serikali imesitisha mishahara ya watumishi wote ambao muundo wa utumishi wao uliwataka kuwa na sifa ya kufaulu kidato cha nne wakati wanaajiriwa lakini hawakuwasilisha vyeti vyao kuhakikiwa na Baraza la Mitihani.

“Tunasitisha mishahara yao kuanzia mwezi Julai hadi hapo watakapowasilisha vyeti vyao kuhakikiwa,” alisema Dk. Ndumbalo.

Dk. Ndumbalo aliongeza kuwa kwa watumishi walioajiriwa wakiwa darasa la saba kabla ya waraka wa Utumishi wa Umma namba moja wa mwaka 2004 uliowataka waajiriwa kuwa na sifa ya kidato cha nne, wataendelea na kazi mpaka watakapostaafu.

Alisema sera ya Menejimenti na Ajira katika utumishi wa umma toleo la mwaka 1998 lilianza kutekelezwa Mei 20, 2004 hivyo kwa walioajiriwa kabla ya hapo warudishwe kazini kama waliondolewa kimakosa.

“Nasisitiza kuwa watumishi wote wa umma walioajiriwa kwa sifa ya elimu ya darasa la saba kabla ya Mei 20 hawahusiki na uhakiki wa vyeti vya kufaulu mtihani wa kidato cha nne na wataendelea kuwa watumishi wa umma katika vyeo vyao mpaka watakapostaafu kazi,” alisema Dk.Ndumbalo.

Aidha alisema serikali inatangaza ajira mpya 10,184 katika sekta mbalimbali huku ikitoa ajira 3,172 kwa sekta ya afya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here