23.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

391 kulipwa fidia ya Sh bil 2.5 na mradi wa bomba la mafuta

Na Allan Vicent, Tabora

Serikali imezindua zoezi la ulipaji fidia kwa wanavijiji 391 waliopo katika maeneo yatakayopitiwa na mradi wa bomba la mafuta unaotarajiwa kutekelezwa hivi karibuni kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga hapa nchini.

Zoezi hilo limezinduliwa jana na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani katika kijiji cha Sojo kata ya Igusule wilayani Nzega mkoani Tabora.

Alisema maandalizi na taratibu zote za ulipaji fidia kwa wahusika zimekamilika na sasa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kampuni ya East African Crude Oil Pipeline (EACOP) yupo tayari kulipa fidia kwa walengwa wote.

Alisema jumla ya wanavijiji 391 watakaopitiwa na mradi huo katika mikoa 8 hapa nchini watalipwa kiasi cha sh bil 2.5 ambapo wakazi 44 ni wa kijiji cha Sojo na watalipwa jumla ya sh mil 424.8.

‘Leo nimezindua rasmi zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wote ambao maeneo yao yatapitiwa na mradi huu, nataka zoezi hili lifanyike haraka iwezekanavyo ili shughuli nyingine zianze mara moja’, alisema

Alibainisha kuwa gharama za mradi huo kutoka Misenyi mkoani Kagera hadi Chongoleani Tanga ni takribani Sh bilioni 28.26 na bomba hilo litakuwa na urefu wa km 1443 kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani-Tanga hapa nchini.. 

Hata hivyo Waziri aliagiza zoezi hilo lifanyike haraka iwezekanavyo huku akisisitiza kila mlengwa kulipwa kiasi kilichoko katika mkataba wake ili kuepusha malalamiko.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk. James Matalagio alisema zoezi la ulipaji fidia litafanyika kwa wananchi wote waliopitiwa na mradi huo.

Alibainisha kuwa jumla ya wanajiji 391 watalipwa fidia ya kiasi cha Sh bililioni 2.5 ambapo miongoni mwa wanufaika hao ni wanakijiji 44 wa kijiji cha Sojo ambao tayari wameanza kusaini mikataba ya fidia zao kiasi cha Sh mil 424.8.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) Martin Tiffen alisema kuwa zoezi la ulipaji fidia kwa wahusika linatarajia kukamilika ndani ya wiki mbili kuanzia sasa na baada ya hapo shughuli nyingine za ujenzi wa mradi zitaendelea.

Aliwahakikishia Viongozi wa Mkoa wa Tabora kuwa zoezi hilo litakamilika kwa wakati na kuwataka wale wote wakaokuwa na malalamiko kuyawasilisha kwa uongozi au kamati ya malalamiko ili yashughulikiwe haraka kabla ya kuanza kulipa fidia.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dk. Batilda Buriani alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa mradi huo, huku akibainisha kuwa mradi huo ni mkombozi kwa uchumi wa wananchi wa mkoa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,244FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles