23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

2nice Mnyama: Wema Sepetu, Mobetto wajipange, Mondi, Kiba Canada wapo juu

SWAGGAZ RIPOTA

KUTOKA jijini Edmonton Alberta nchini Canada, rapa Mulumba Alphonse maarufu kama 2nice Mnyama, ameendelea kuiwakilisha vyema Afrika Mashariki kwa nyimbo zake kutikisa chati za muziki nchini humo.

Rapa huyo amekuwa akichanganya ladha ya muziki wa  Afrika na ule wa Magharibi kwa kuwatumia watayarishaji kutoka Tanzania, Afrika Kusini, Nigeria, Canada, Uingereza na Marekani.

Akiwa katika harakati za kutangaza muziki wake Afrika, 2nice Mnyama, amefanya mahojiano yafuatayo na Swaggaz kuhusu muziki na maisha yake  ili mashabiki waweze kumfahamu zaidi, karibu.

Swaggaz: 2nice Mnyama ni nani na uliingia vipi kwenye muziki?

2nice Mnyama: Mimi nimezaliwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika familia ya watoto 10 na mimi peke yangu ndiyo nimebahatika kuwa na kipaji cha muziki.

Nilikimbia Kongo kwa sababu ya vita kwa hiyo nikakimbilia Kigoma, Tanzania ambako huko ndiyo nilikulia na baadaye nikaja Canada. Safari ya muziki ilianza mwaka 2008 kule Afrika Kusini ambako kwa mara ya kwanza ndiyo niliingia studio kurekodi.

Swaggaz: Kuna changamoto zozote unakutana nazo wakati ukifanya muziki wako nje ya Afrika?

2nice Mnyama: Changamoto zipo lakini kubwa ni kwamba mimi nafanya kazi na maprodyuza wazungu ambao mwisho wa siku nikiwa narekodi hhuwa hawaelewi ninachoimba ila wanadata sana na midundo ya kiafrika hata kama hawaelewi ninachoimba, wazungu wanafurahi na wanapenda midundo ya kiafrika.

Swaggaz: Umefanya nyimbo nyingi, je mpaka sasa umepata mafanikio gani?

2nice Mnyama: Nimepata mafanikio mengi, kupata umaarufu ndani na nje ya Canada. Hii ngoma yangu mpya Go Dow Low imenifungulia milango ya kolabo mbalimbali, wasanii wanahitaji kunishirikisha. Pia kwenye mitandao ya kuuza muziki kama iTunes na Spotify tunashukuru Mungu tunapata fedha, watu wanapagawa na video na kila kitu kinakwenda sawa.

Swaggaz: Hapa Bongo tumeshaona mavideo vixen wengi huwa wanalazimika kutoka kimapenzi na wa wasanii baada ya kazi, kwa upande wako ipo vipi?

2nice Mnyama: Hiyo ipo ila kwa upande wangu mimi siwezi kutoka na mavideo vixen, kwasababu hii ni kazi na nina waheshimu, kutokana na heshima ninayowapa na wao pia wananiheshimu.

Swaggaz: Unatamani kufanya kazi na mastaa gani Afrika?

2nice Mnyama: Mimi ni msanii mkubwa hapa Canada, sasa hivi natamani sana muziki wangu ufike Afrika kwa hiyo mastaa ambao natamani kufanya nao kazi ni Davido, Wizkid, Casper Nyovest, Diamond Platnumz, Ali Kiba, Harmonize, Vanessa Mdee na wengine maana kupitia ukubwa wao nitatimiza lengo langu.

Swaggaz: Unaweza vipi kufanya kazi na prodyuza tofauti tofauti duniani?

2nice Mnyama: Teknolojia imerahisisha mambo, kwa mfano hapo Tanzania ninafanya kazi na prodyuza wa Harmonize, Fraga ambaye huwa ananitumia biti, naingiza sauti kwenye studio za huku na kuzifanyia ‘mixing’ na ‘mastering’ kisha ngoma inatoka ikiwa kali.

Swaggaz: Jambo gani huwezi kusahau katika safari yako ya muziki?

2nice Mnyama: Siwezi kusahau mara ya kwanza kuingia studio Afrika Kusini, nilikuwa mwoga sana kiasi cha kusahau mistari mara kwa mara hadi prodyuza ananigombeza lakini ile hali iliisha.

Swaggaz: Hapa Bongo mastaa kama Wema Sepetu na Hamisa Mobetto vipi hapo Canada?

2nice Mnyama: Hao wadada kina Wema na Mobetto hapa Canada wanazungumzwa zaidi na Waafrika waliotoka Kenya, Uganda, Rwanda, Kongo, Burundi na wale wanaoongea Kiswahili lakini wazungu hawawajui labla mzungu mmoja mmoja.

Swaggaz: Na vipi kuhusu nguvu ya Diamond na Ali Kiba nchini Canada?

2nice Mnyama:Diamond na Ali Kiba ni watu wanaokubalika sana hapa Canada, Diamond aliwahi kufika mpaka huku Edmonton kupiga shoo ila Ali Kiba aliishia Tolonto hakufika huku kwetu. Watu wote yaani wazungu na waafrika wanawakubali na wanawazunguzia vizuri hawa jamaa wapo juu.

Swaggaz:Mipango yako mwaka huu kwenye muziki ni ipi ?

2nice Mnyama: Kwanza nahitaji niende Kimataifa zaidi, pili naomba Mungu anisaidie nifanye kolabo na wasanii wakubwa, tatu ‘fanbase’ yangu izidi kuwa kubwa kila kukicha na soko langu liwe zuri nikiweka ngoma watu ‘wa-stream’ kwa wingi.

Swaggaz: Asante kwa muda wako.

2nice Mnyama: Shukrani sana, mashabiki zangu wa Afrika Mashariki waendelee kunipa sapoti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles