25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

2016: MWAKA WA MAVUNO, NJAA KWA WAPENDA VITA

RIPOTI ya Shirika la Chakula Duniani (FAO) mwaka 2017 inaeleza kuwa uzalishaji wa nafaka duniani kwa ujumla ulipiga hatua kubwa mwaka 2016.

Ahueni hiyo hata hivyo iko zaidi kwa nchi za Amerika ya Kati, wakulima wakubwa wa Asia, Ulaya na Amerika ya Kaskazini.

Ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Machi 2, 2017 ya matarajio ya mazao na hali ya chakula.

Kwa ujumla ripoti inasema makusanyo ya chakula duniani ni mazuri ukiachilia mbali tatizo la upatikanaji na mgawanyiko katika maeneo yenye vita za wenyewe kwa wenyewe.

Aidha, ilisema ukame unazidi kuongezeka katika usalama wa vyakula kwenye maeneo ya nchi za Afrika ya Mashariki.

Nchi 37 ziliomba msaada wa chakula na kati ya hizo 28 ni nchi za Afrika, ambazo ukame umedumu kwa muda mrefu kutokana na janga la mvua za Elnino, lililosababisha uvunaji mdogo kwa mwaka 2016.

Pamoja na hayo, hata kama kuna matokeo mazuri ya mavuno kwa upande wa kilimo cha Afrika ya Kusini, ukiondoa kwenye vurugu na ghasia zinazosababisha ongezeko la wenye uhitaji wa msaada wa chakula.

Kwa sasa Sudan ya Kusini inaongoza kuwa na dharura ya usalama na chakula sambamba na nchi za Nigeria, Somalia na Yemen.

Ni hali ambayo haijawahi kutokea kabla kukabiliana na hali ya njaa na machafuko kwa wakati mmoja, yaani matukio yote mawili kufuatana.

Hayo ni maneno ya Kostas Stamoulis, ofisa katika Ofisi ya Mkurugunzi Mkuu na Mkuu wa ofisi ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii wa FAO.

Anaongeza, hii ni hali ambayo inahitaji hatua za haraka ili kuweza kutoa huduma ya chakula na hata zana za kuweza kuwasaidia kwa kuzuia aina nyingine inayoweza kujitokeza katika maisha endelevu.

Nchini Sudan, watu 100,000 wanakabiliwa na njaa katika mikoa ya Leer na Mayendit.

Kwa ujumla ni karibu watu milioni 4.9 na ambao  wamekumbwa na baa la njaa na ukame. Lakini idadi hiyo inakaribia milioni 5.5, ambapo nusu yao kufikia mwishoni mwa Julai mwaka huu wote watakuwa wameathirika vibaya kwa njaa.

Kwa upande wa Nigeria watu milioni 8.1 wako shakani kwa ukosefu chakula, nao wanahitaji kwa haraka chakula  na zana za kuwalinda.

Hali hiyo inajitokeza kutokana ukusanyaji mdogo wa chakula mwaka jana kunakotokana na machafuko ya wanamgambo wa al –Shabaab na kuanguka kwa uchumi wa nchi kulichagizwa na anguko la bei ya mafuta.

Nchini Yemen watu milioni 17 yaani robo tatu ya watu wote wa nchini humo nao wako katika hali mbaya ya ukosefu wa chakula.

Nchini Somalia, vurugu, ghasia na ongezeko la njaa vimeongezeka mara dufu kwa miezi sita na kusababisha takribani ya watu milioni 2.9 kuwa katika hitaji kubwa la chakula.

Wakati ukame ukiwa mchawi mkubwa wa baa la njaa, migogoro na machafuko ya kiraia katika nchi za Afghanistan, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Irak, Myanmar na Syria imesababisha ukosefu wa chakula kwa mamilioni ya watu na kuleta madhara kwa nchi jirani zinazokaribisha wakimbizi.

Licha ya ukame katika Afrika ya Mashariki mwishoni mwa 2016 imeongeza uhaba wa chakula katika nchi mbalimbali za kanda ya kusini.

Kwa mtazamo wa wakati ujao, FAO inatabiri uzalishaji wa ngano kimataifa kwa mwaka 2017 utakuwa na upungufu wa asilimia 1.8 kulinganisha na rekodi ya mwaka jana hasa kutokana na matarajio ya asilimia 20 ya kushuka kwa uzalishaji nchini Marekani.

Hicho ni kiwango cha chini mno cha uzalishaji ngano wakati wa majira ya baridi kwa kipindi cha zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Nchini Brazil na Argentina kwa mwaka huu matarajio ya zao la mahindi ni chanya kwa ujumla katika eneo lote la kusini mwa dunia.

Kwa upande wa kilimo cha mpunga, hali ni mchanganyiko, lakini bado ni mapema mno kufanya utabiri sahihi kwa ajili ya wingi wa mazao muhimu zaidi duniani.

Uzalishaji wa mahindi nchi za kusini mwa Afrika umepunguzwa kutokana na mvua za El Nino, lakini nafuu kidogo itakuwa mwaka huu baada ya kuwapo dalili ya ongezeko la asilimia 50 ukilinganishwa na mwaka jana.

Hata hivyo, kuna dalili za wadudu waharibifu pamoja na mafuriko nchini Msumbiji, Zambia na Zimbabwe, ambavyo vinaweza kuzuia faida za uzalishaji kwa mwaka 2017.

Ripoti hiyo ya inakuja baada ya mwezi uliopita FAO kuonya kwamba lengo la Jumuiya ya Kimataifa kufuta baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2030 huenda lisifikiwe kutokana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza kwa sasa duniani.

Kumekuwapo na matumizi makubwa ya rasilimali za dunia kupita kiasi; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa usawa kati ya watu.

Mbinu mkakati ya uhakika wa usalama wa chakula duniani ilishafikiwa takribani miaka 30 iliyopita, lakini athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya mambo mapya yanayotishia usalama wa maisha ya watu wengi duniani.

Kumekuwapo na uharibifu mkubwa wa misitu kwa matumizi ya binadamu, hali ambayo imesababisha kukauka kwa vyanzo vya maji sehemu mbalimbali za dunia na hivyo kusababisha ukame unaoendelea kutishia usalama wa maisha ya mamilioni ya watu duniani.

“Kama huu ndio utakaokuwa mwelekeo kwa Jumuiya ya Kimataifa, kuna hatari kubwa kwa siku za usoni kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula,” anasema Profesa Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi Mkuu wa FAO.

Ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu duniani inakadiriwa kufikia bilioni 10 na hivyo kutakuwapo uhitaji mkubwa wa chakula kwa walau asilimia 50 ya ilivyo sasa, kiasi hata cha kuathiri mfumo wa maisha na chakula katika ujumla wake.

Kutakuwapo ukataji mkubwa wa miti kwa ajili ya matumizi ya binadamu; uharibifu wa mazingira pamoja na uzalishaji mkubwa wa gesi ya ukaa.

Mabadiliko ya tabianchi yatakuwa na athari kubwa katika sekta ya kilimo kutokana na mafuriko pamoja na ukame wa kutisha.

Hata hivyo, FAO inasema dunia inao uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa wote, lakini jambo la msingi ni watu kubadili tabia na mfumo wa maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles