27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

20 WAJITOKEZA KUUAGA MWILI WA MCHORAJI NEMBO YA TAIFA

 

 

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WATU takribani 20 jana walijitokeza kuuaga mwili wa anayedaiwa kuwa mbunifu wa nembo ya Taifa ya bibi na bwana, Francis Maige maarufu Ngosha, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu kabla ya mauti kumfika Mei 29, mwaka huu.

Miongoni mwa watu waliojitokeza kuuaga mwili huo, ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Publishers, Erick Shigongo na mchoraji maarufu wa vibonzo, Nathan Mpangala.

Wengine ni Mkurugenzi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi (Tafca), Adrian Nyangamalle na Msajili wa Taasisi zisizo za kiserikali (NGO's) wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Marcel Katemba.

Akizungumza wakati wa kuuaga mwili huo, Mkurugenzi wa Huduma za Dharura wa Muhimbili, Dk. Juma Mfinanga, alisema uchunguzi ulibaini kwamba alikuwa akiugua kifua kikuu (TB).

“Inaonesha TB hiyo alikuwa nayo kwa muda mrefu na kwa kuwa alichelewa hospitalini, ilikuwa imekula mno ndani ya mwili wake, alikuwa na maumivu ya kifua, tulijitahidi kuokoa maisha yake lakini haikuwezekana,” alisema.

Alisema mzee huyo alikuwa na miaka 86 na kwamba alikosa lishe na malezi bora.

“Kitaalamu mzee akikosa lishe inayotakiwa na malezi bora, ni rahisi kupata magonjwa mengi nyemelezi ikiwamo TB, ni vema watu wakajenga tabia ya kupima afya zao na wazee wapewe malezi bora,” alisema.

Kutokana na kuibuka utata wa nani hasa ni mchoraji wa nembo ya Taifa, akizungumza katika shughuli ya kuaga mwili wa Ngosha, Mkurugenzi wa Basata, Mngereza, alisema kuanzia sasa Serikali itahakikisha wasanii wote wanafuata utaratibu ili watambulike na kazi zao.

“Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ameniagiza pia kukabidhi ubani wa Sh 300,000 ambazo atakabidhiwa muuguzi anayeondoka na msafara kwenda Mwanza akazifikishe kwa familia ya marehemu,” alisema.

Naye mchora vibonzo Mpangala alisema wakati umefika kwa Serikali kufanya utafiti wa kutosha kupata taarifa sahihi za watu waliosaidia Taifa kwa kubuni na kuchora vitu mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles