24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

Watetezi haki za binadamu walaani polisi

Onesmo ole Ngurumwa
Onesmo ole Ngurumwa

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umelaani kushikiliwa na polisi kwa watetezi wa haki za binadamu na wafugaji, kwa zaidi ya siku 10 bila dhamana.

Katika taarifa yake   jana, asasi za  raia zimekemea vikali  kushikiliwa  wakili wake na kujumuishwa katika tuhuma za washitakiwa.

Asasi hizo ni   Chama cha Wafugaji Tanzania, Baraza la Asasi za Kiraia Tanzania (NACONGO) na  Vyama vya  Wanasheria vya Tanganyika na Zanzibar.

Kwa mujibu wa taasisi hizo, tukio hilo ni kunyimwa haki ya uwakilishi kwa watuhumiwa na kumkosesha wakili kufanya kazi yake.

Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa,   a watu hao wanashikiliwa kwa madai ya ujasusi katika Kituo cha Polisi Loliondo, mkoani Arusha.

“Asasi za  raia zinakemea matukio hayo kwa kuwa yanakiuka haki za binadamu na yanavunja Katiba ya mwaka 1977,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema baada ya mtandao kufuatilia kwa vyombo vya usalama mkoani Arusha, timu inayoendesha operesheni Loliondo inaongozwa na polisi kwa kushirikiana na vikosi vingine vya usalama.

Ilidaiwa kuwa Julai 21, mwaka huu, mtandao kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ulituma wakili  Shilinde Ngalula   na waandishi kufuatilia ukiukwaji huo na   kuwapa uwakilishi wa uwakili watetezi waliobaki ndani kwa takriban siku tisa sasa.

“Cha ajabu wakili tuliyemtuma naye alifukuzwa asisikilize mahojiano.  Hata hivyo Julai 22 mwaka huu alikamatwa na kuunganishwa na watuhumiwa wengine,”  ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema watetezi na wanaharakati  wanane wameendelea kushikiliwa na kunyimwa dhamana huku watuhumiwa wengine wenye vyeo vya  siasa wakipewa dhamana katika tuhuma hizo.

Taarifa hiyo iliwaeleza   watetezi wa haki za wafugaji Loliondo wanaondelea kuwa chini ya ulinzi kuwa ni Samweli Nangiria, Supuk Olemaoi,  Clinton Kairung na Yohana  Mako.

Ilidaiwa matukio ya ukiukwaji haki na kukamatwa kwa watetezi wa haki za binadamu yamekuwa yakiendelea kujitokeza huku kukiwa na vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wa serikali kwa asasi za kiraia.

“Watetezi tunaikumbusha Serikali na vyombo vyake hasa Jeshi la Polisi kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya Mwaka 1977 inataka vyombo vyote vya Serikali  kuhakikisha   utu na haki nyinginezo za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa kwa mujibu wa Ibara ya 9 (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles