25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Maji ya chupa yamponza mhandisi

Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bahi, Deus Mchele akisikiliza maoni ya wananchi katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mchito mkoani Dodoma.
Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bahi, Deus Mchele akisikiliza maoni ya wananchi katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mchito mkoani Dodoma.

Na RAMADHAN HASSAN, BAHI

MAJI ya kunywa ya chupa yamemtokea puani Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bahi mkoni Dodoma, Deus Mchele,   alipojikuta katika wakati mgumu baada ya kunywa maji hayo kwenye  mkutano wa Kijiji cha Mchito.

Kitendo hicho kilizua vurugu kwa wanakijiji hao kuja juu wakisema mhandisi huyo wa maji   ameonyesha dharau kwao.

Walisema    hawajawahi kunywa hata  maji ya bomba au kisima kisafi tangu kianzishwe kijiji hicho.

Tukio hilo lilitokea juzi katika kijijini hapo wakati Mhandisi Mchele, alipokuwa ameongozana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Benardetha Januari.

Wote kwa pamoja walijikuta wakiwashiwa moto na wananchi kutokana na tukio hilo.

Viongozi hao walikwenda katika kijiji hicho kuzungumza na wananchi kuwaeleza sababu za  kukwama   mradi wa maji kijijini hapo kwa zaidi ya miaka mine.

Katika kikao hicho, Mhandisi Mchele  alikuwa amebeba chupa ya maji safi ya Uhai na  kila wakati  alikuwa akiinyanyua na kunywa, hali iliyoanza kuzua minong’ono ya chinichini kutoka kwa wananchi.

Dakika tano baada ya kufika viongozi hao,  alisimama Mwenyekiti wa Kijiji cha Mchito, Moses Daniel  na kufungua mkutano huo kabla ya kumpa fursa Diwani wa Kata wa hiyo, Mathew Malilo (CCM), ambaye moja kwa moja aliruhusu maswali kutoka kwa wananchi.

Ilipotolewa fursa hiyo, alisimama mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Ashery Mtonga ambaye ‘alimlipua’ mhandisi Mchele  akidai kuwa alikuwa ameonyesha dhararu kubwa kwao kwa kwenda na chupa ya maji wakati kijiji hicho hakijawahi kuona maji ya bomba kwa zaidi ya miaka mitano.

“Nyie mnakuja na maji ya chupa watoto wetu je? Mradi wa maji katika kijiji hiki  una miaka minne hatujawahi kuona hata tone la maji… sisi leo (juzi) tunataka mtuambie maji yataanza kutoka lini.

“Kila kukicha tunakunywa maji ya madimbwi ambayo nayo hukauka. Nyie hapo mmekuja na maji ili tuwaone mnavyofaidi… jamani hii kweli ni haki?” alihoji Mtonga.

Naye Jemima Soweya, alisema alishangazwa na mhandisi huyo kwenda na maji huku wao wakiwa hawajui hatima yao na kila wakati hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

Mhandisi Mchele alipopewa nafasi ya kutoa ufafanuzi kuhusu mradi huo wa maji,   alisema  wilaya ilitoa kazi ya utengenezaji wa mradi huo kwa Kampuni ya Intersystem Holding Company Ltd mwaka 2012.

Alisema hadi  sasa imeshindwa kukamilisha kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano.

Kutokana na hali hiyo ilibainika mkandarasi huyo wa mradi wa maji alishindwa kuutekeleza  kwa wakati hivyo ikaamuriwa afukuzwe na yeye akawasilisha makakamiko ya kutaka alipwe Sh milioni 100.

“Baada ya kuleta malalamiko tukaona hatuwezi kumpa mkataba mtu mwingine mpaka tujadiliane tupate majibu ya mgogoro huu.

“Ila kwa kweli mkandarasi yule hakuwa na uwezo wa kujenga mradi huu. Na mradi huu ulikuwa unatekelezwa kwa gharama ya Sh milioni 246 na tayari tulikuwa tumeshamlipa robo tatu ya fedha,” alisema.

Mchele alisema hajalala kwa vizuri miaka minne sababu ikiwa ni mradi huo wa maji wa Mchito kutokukamilika.

Maelezo hayo   yaliamsha hasira kwa wananchi na akasimama mwananchi mmoja, Anderson Ndelele aliyehoji   kama mhandisi huyo wa wilaya hajalala kwa miaka minne  angekuwa hai mpaka sasa?

“Leo mngeona aibu hata kuja na hayo maji ya chupa tena unatuambia hujalala kwa muda wa miaka minne ungekuwa hai kweli si unatudanganya!

“Nyie endeleeni na kesi yenu sisi tunataka maji leo (juzi)… hamuondoki mpaka tupate maji, semeni maji yatatoka lini hapa Mchito,’’alisisitiza  Ndelele,

Alipotakiwa kutoa majibu ya maswali hayo, Mhandisi Mchele aligoma akisema hakuwa na majibu hali iliyomlazimu diwani Malilo  kuwatuliza wananchi hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles