Na Mwandishi Wetu, Geita
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo za rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Amesema siku zote umekuwapo ushirikiano mzuri kati ya Serikali na asasi mbalimbali yakiwamo madhehebu ya dini katika kuwapatia huduma za jamii kama vile, afya, elimu, maji, utunzaji wa mazingira na nyingi nyingine.
Majaliwa aliyasema hayo jana alipomuwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika Ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa Mhashamu Askofu Flavian Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita.
“Serikali inatambua jitihada kubwa zilizowekwa na Kanisa Katoliki katika Jimbo hili la Geita na Tanzania kwa ujumla, hivyo wito wangu kwa Baba Askofu na waumini wa kanisa kwa ujumla wenu ni kuwaomba muendelee na kazi hii nzuri ya kutoa huduma muhimu kwa jamii,” alisema.
Alisema maendeleo ya nchi yanawategemea wote hivyo ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali utawezesha maendeleo ya taifa kupatikana kwa kasi zaidi na kunufaisha wananchi wote.
Jukumu la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ambayo yatasaidia Mtanzania kujikomboa na umaskini na kazi kubwa ya viongozi wa dini ni kuunganisha jamii na siyo kuwatenganisha, alisema.
Waziri Mkuu alisema kinachotakiwa kufanywa na wote ni kumwuomba Mwenyezi Mungu awawezesha kuwaelewa viongozi walioko madarakani na kutii maelekezo yanayotolewa kwani hata vitabu vya dini vinaelekeza kutii mamlaka.
Alisema iwapo waumini watatii na kuzingatia mafundisho ya roho yanayotolewa na viongozi wao wa dini ni dhahiri yatajenga imani miongoni mwao na upendo utatawala katika jamii nzima.
Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote katika kuwahudumia Watanzania wote bila ubaguzi.