Oscar Assenga, Tanga
Watu 10 wamenusufika kifo huku mmoja akiwa hajulikani alipo baada ya boti waliyopanda kuzama kwenye Bahari ya Hindi Jijini Tanga, walipokuwa wakienda kuangalia visiwa vilivyopo baharini humo.
Akizungumza leo na Mtanzania Digital leo Jumatatu Agosti 12, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema limetokea jana ambao walikuwa watu hao walikuwa wamepanda boti waliyokodi kutoka eneo la Yatch Club.
“Baada ya watu hao kupanda boti hiyo, ambao walikuwa wakienda kutembelea visiwa mbalimbali vilivyopo kwenye bahari hiyo na ndipo upepo mkali uliwazuia kwenda mbele na walipotaka kugeuza kurudi walipotoka ndipo ilipopinduka na kuwamwaga.
“Kwenye boti hiyo kulikuwa na watu 11 ambapo 10 kati yao waliokolewa kutokana na kuvaa maboya wakati wakiwa baharini na mwingine mmoja ambaye inadaiwa hakuwa nayo hadi sasa hajulikani alipo,” amesema.
Aidha, Kamanda Bukombe ametoa wito kwa wananchi wanaotumia bahari kusafiria kuchukua tahadhari wanapokuwa baharini kwa kuhakikisha wanavaa maboya ya kujiokolea ili wakati yanapotokea majanga kama hayo waweze kuona namna ya kujiokoa.