30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ukerewe yageuka uwanja wa mapambano dakika 45

PETER FABIAN – UKEREWE

WATUHUMIWA ujambazi wanane wameuawa wilayani hapa, katika tukio la kushambuliana kwa risasi na polisi waliokuwa wanawafuatilia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana, alisema tukio hilo lililodumu kwa dakika 45 lilitokea saa 7:40 usiku katika daraja linalounganisha vijiji vya Bukima na Igala wakati watu hao walikuwa katika mpango wa kwenda kufanya uvamizi.

Shana alisema walipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema na zile za kitengo cha kiintelejensia kwamba kuna watu wanapanga njama za kufanya uhalifu wa kutumia silaha nyakati za usiku katika maeneo mbalimbali ya Kisiwa cha Ukerewe, ndipo wakatuma kikosi maalumu kufanya doria kali na kuweka mtego uliofanikiwa kuwaua na kukamata silaha.

 “Majambazi hao walipoona gari la polisi wakiwa eneo la Darajani walifyatua risasi kuwatisha, lakini polisi walikuwa wamejipanga kukabiliana nao na kujibu mapigo na katika majibizano ya risasi yaliyodumu kwa dakika 25, askari walifanikiwa kuwaua majambazi watano papo hapo na wengine watano walifanikiwa kutoroka,” alisema.

Shana alisema wakati polisi wakiendelea kupekua maiti za watu hao waliwakuta na bunduki moja aina ya shot-gun (iliyotengenezwa kienyeji) na maganda kadhaa ya risasi, panga moja, nondo moja na simu sita za mkononi.

 “Wakati askari wakiwa eneo walilouawa majambazi hao, alifika kijana mmoja aitwaye Mateso Nyagabona, mwendesha bodaboda ambaye pia ni mkazi wa Kijiji cha Bukima na kuwaeleza askari kwamba amekutana na watu watano katika Kijiji cha Bwasa waliomshambulia kwa kumpiga nondo, lakini alifanikiwa kukimbia,” alisema.

Shana alisema baada ya taarifa za Nyagabona, polisi waliondoka kuwafuatilia na wengine kuendelea kubaki eneo la tukio na walipofika Bwasa saa 9:05 usiku majambazi hao watano walipowagundua walianza tena kuwarushia risasi.

 “Polisi walikuwa wamejiandaa na kukabiliana nao kwa kuvaa mavazi maalumu yasiyopenyeza risasi na kuanza kukabiliana nao kwa dakika 20 na licha ya kurusha risasi walikimbilia mlimani kwa lengo la kujificha kwenye mapango ya mawe, lakini askari walifanikiwa kuwaua majambazi wengine watatu, huku wawili wakifanikiwa kutoroka,” alisema.

Pia alisema baada ya kuwapekua waliwakuta wakiwa na silaha moja ya kivita aina ya AK 47, magazini mbili, risasi 15, panga moja, nondo moja na simu nne za mkononi.

 “Licha ya kuwaua majambazi wanane, pia tumefanikiwa kukamata bunduki mbili na simu 10 za mkononi, huku kati ya hizo, nne zikiwa zimeporwa kwa wananchi katika matukio ya uhalifu ya Desemba, mwaka jana na Januari, mwaka huu,” alisema.

Shana alisema bado polisi wanaendelea kuwatafuta wawili waliofanikiwa kutoroka huku miili ya wengine wanane waliouawa ikiwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe, mjini Nansio na kutoa fursa ya wananchi kujitokeza kuwatambua.

“Majambazi wote wanane waliouawa tumewakuta na karatasi ya orodha ya majina ya wafanyabiashara na watu mbalimbali waliokuwa wamepanga kuwavamia, wakiwamo wenye maduka makubwa na ya kati, mashine za kusaga, vituo vya mafuta, magari ya kubeba abiria na wanaojishughulisha na uvuvi ndani ya Ziwa Victoria, miamala ya fedha za kampuni za simu za mkononi na mawakala wa taasisi za fedha,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Boniphace Magembe, alimpongeza Shana na polisi waliofanikiwa kuwaua watuhumiwa hao wa ujambazi kabla hawajaleta maafa na kupora mali za wananchi wa maeneo mbalimbali ya Ukerewe na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri kwa watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles