23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Array

Saratani ya utumbo mpana yatesa vijana

Na VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM

TATHMINI ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) imeonesha kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 30 linateswa zaidi na saratani ya utumbo mpana (Colorectal cancer) kuliko makundi mengine katika miaka ya hivi karibuni.

Saratani hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ulaji usiofaa hususan nyama nyekundu yenye mafuta mengi, nyama ya kuchoma, vyakula vyenye  chumvi nyingi na vilivyosindikwa.

Hali hiyo ni tofauti na miaka ya zamani ambapo kundi la watu wazima wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea ndilo ambalo lilionekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya wanaougua ugonjwa huo.

Hayo yalielezwa na Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani na Elimu kwa Umma, Dk. Maguha Stephano alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

 “Visababishi vinavyochangia mtu kuwa kwenye hatari ya kupata saratani hiyo ni pamoja na ulaji usiofaa, hususan nyama nyekundu yenye mafuta mengi, nyama ya kuchoma, vyakula vyenye  chumvi nyingi na vilivyosindikwa.

“Vingine ni uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na wakati mwingine mtu huweza kupata saratani hiyo kutokana na kurithi ndani ya familia.

 “Mtu anapaswa kula nyama ili kujenga mwili, lakini inashauriwa nyama hiyo isiwe yenye mafuta mengi, wataalamu wa lishe wanashauri kwa wiki mtu ale angalau nusu kilo ya nyama na si zaidi.

“Nyama choma ni hatari kiafya kwani inapochomwa ule moshi huwa na kemikali nyingi kwa mfano ‘kaboni-monoksaidi’.

“Zile kemikali (sumu) zinapoingia mwilini huweza kusababisha mabadiliko kwenye chembe chembe hai za mwili, hatimaye mtu huishia kupata saratani ya utumbo mpana,” alisema Dk. Stephano ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani wa ORCI.

Aidha Dk. Stephano alisema nyama za kusindikwa kwa mfano soseji mara nyingi huwa zinawekwa mafuta mengi, chumvi nyingi na vitu mbalimbali kuzuia zisiharibike.

Dk. Stephano alisema kutokula mbogamboga na matunda nayo ni sababu inayochochea mtu kujiweka kwenye hatari ya kupata saratani hiyo, unene uliokithiri na kutokufanya mazoezi.

“Hivyo tunashauri jamii kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kuepuka unywaji wa pombe, uvutaji sigara na kufanya uchunguzi wa afya wa mara kwa mara, hapa ORCI tunafanya, waje wakati wowote,” alisema Dk. Stephano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles