MWANDISHI WETU-GENK
MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, amefunga bao moja wakati timu yake ya
KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya Royal Antwerp FC katika mchezo wa
Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji uliochezwa juzi Uwanja wa Luminus Arena, Genk.
Samatta
alifunga bao lake dakika ya 55, baada ya kiungo wa kimataifa wa Ukraine, Ruslan
Malinovskiy, kufunga la kwanza kwa penalti dakika ya 25, kabla ya mshambuliaji
Mjapan, Junya Ito, kufunga la tatu dakika ya 57 na kiungo Mbelgiji, Bryan
Heynen Heynen, kufunga la nne kwa penalti dakika ya 90.
Ushindi huo unaifanya Genk ifikishe pointi 50 katika hatua ya pili ya Ligi ya Ubelgiji na kuendelea kuongoza, ikifuatiwa na Club Brugge yenye pointi 41.
Samatta sasa amefikisha mabao 23 msimu huu na la tatu katika hatua ya pili ya ligi hiyo, akiwa anaendelea kuongoza kwenye mbio za ufungaji bora.
Kwa ujumla, Samatta mwenye umri wa miaka 26, ameifungia Genk mabao 62 katika mechi 153 za mashindano yote, tangu alipojiunga na timu hiyo Januari mwaka 2016, akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika ligi ya Ubelgiji pekee, amefunga mabao 47 katika mechi 120, Kombe la Ubelgiji mabao mawili katika mechi tisa na Europa League mabao 14 katika mechi 24.