30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ni bajeti ya uchaguzi

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SERIKALI imetoa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti ya mwaka 2019/20, ambapo Sh trilioni 33.105 zinatarajiwa kukusanywa huku Sh trilioni 20.856 zikitengwa kwa matumizi ya kawaida ikiwamo uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu mwakani.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akisoma mpango huo mbele ya wabunge mjini Dodoma, alisema matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 12.248, ambapo Sh trilioni 9,737.7 ni fedha za ndani na Sh trilioni 2.510.9 ni fedha za nje.

Alisema kwa kuzingatia sera ya bajeti kwa mwaka 2019/20 sura ya bajeti inaoenesha kuwa jumla ya Sh trilioni 33.105 zinatarajiwa kukusanywa.

Alisema mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 23.045.

Alisema mikopo ya ndani inakadiriwa kuwa Sh trilioni 4.960 na mikopo ya nje yenye ya kibiashara Sh trilioni 2.316  na misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo Sh trilioni 2.783.

 UTEKELEZAJI WA BAJETI ILIYOPITA

Alisema katika mwaka 2018/19 Serikali ilitenga Sh trilioni 12.007 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, zikijumlisha Sh trilioni 9.876 fedha za ndani na Sh trilioni 2.130 fedha za nje.

Alisema hadi Januari 2019 jumla ya Sh trilioni 2.788  ndizo zilizotolewa kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo.

Aidha Sh bilioni 144 zilipokelewa  kutoka kwa washirika wa maendeleo  na kupelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo  inayotekelezwa kwenye wizara, taasisi na wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa .

Dk. Mpango alisema Sh trilioni 3.803.4 zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali  ya maendeleo.

“Serikali imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha Sh trilioni 1.433.8 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo mradi wa kufufua umeme kwa nguvu ya maji ya Mto Ruvuma,”alisema Dk. Mpango.

VIPAUMBELE

Waziri Dk. Mpango alivitaja vipaumbele katika bajeti hiyo ni vinne ambavyo ni  viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda.

Alisema miradi inayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususani kilimo madini na gesi asilia.

Dk. Mpango alisema miradi hiyo ni pamoja na kiwanda cha kuchakata gesi asilia, uanzishwaji na uendelezaji wa kanda maalum za kiuchumi na kongane za viwanda ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na uvuvi.

Kipaumbele cha pili, Dk Mpango alisema ni kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

Alisema miradi itakayotekelezwa ni ile yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi, upatikanaji wa chakula na lishe bora na huduma za maji safi na salama.

“Shughuli zinazotiliwa mkazo ni pamoja na kugharimia utoaji wa elimu msingi bila ada, kupunguza vifo vya mama vinavyotokana na uzazi utekelezaji wa Programu ya maendeleo  ya sekta ya elimu,ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi nchini pamoja na kuboresha huduma za maji vijijini,”alisema Dk Mpango.

Waziri huyo wa Fedha na Mipango alikitaja kipaumbe cha tatu kuwa ni uboreshaji wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji.

Alisema miradi itakayotekelezwa ni ile yenye lengo la kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu(reli, barabara, nishati, viwanja vya ndege).

Aliitaja miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kufufua umeme wa maji Rufiji MW 2,115, kuboresha Shirika la Ndege Tanzania,Ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge na uendelezaji  wa mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara  na uwekezaji.

WAZIRI MKUU

Kwa upande wake,Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa awali akimkaribisha Waziri wa Fedha na Mipango ili aweze kuwasilisha taarifa hiyo, aliwataka mawaziri kuhudhuria vikao vya kamati ili kurahisisha shughuli za Bunge ziweze kwenda vizuri.

“Baada ya hapa kutakuwa na vikao mbalimbali, mawaziri watatakiwa kuwa wana ripoti katika kamati mbalimbali, nawaomba mawaziri wote kuhudhuria vikao vyote vya kamati.

“Na naamini mawaziri wote watapatikana nafanya hilo ili kurahisisha shughuli zetu na kuwezesha shughuli za bunge ziende kama ambavyo zimepangwa, naamini mtapata ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini,”alisema Waziri Mkuu.

SPIKA NDUGAI

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema lengo la mkutano huo ni kutekeleza matakwa ya kisheria ya kanuni ya 97 kanuni ndogo ya 1 na 2 ya kanuni za Bunge toleo la Januari mwaka 2016.

Alisema kanuni hiyo inaelekeza kwamba Marchi 11 kila mwaka au siku yoyote ya kazi inayofuata Waziri anaehusika na mambo ya mipango atawasilisha kwa wabunge mapendekezo ya Serikali ya mipango ya mwaka wa fedha unaofuata.

Aidha katika tarehe hiyo pia Waziri wa Fedha atawasilisha kwa wabunge mapendekezo ya Serikali kuhusu kiwango na  ukomo wa bajeti wa mwaka unaofuata.

MAONI YA WABUNGE

Wakichangia baadhi ya wabunge walitofautiana na mapendekezo hayo, huku baadhi yakisema ni mazuri na wengine wakidai kwamba hayatekelezeki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Nagwenjwa Kaboyoka alisema mambo yamekuwa yakipangwa vizuri lakini tatizo linakuja kwenye utekelezaji.

Kaboyoka ambaye ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema) alisema taarifa zinaonesha kwamba usambazaji wa maji vijijini umeongezeka wakati kila siku anapokea simu kwamba kuna shida ya maji katika maeneo ya vijijini.

“Tunamdanganya nani wakati tunajidanganya wenyewe ukiangalia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo unakuta eti usambazaji wa maji vijijini umeongezeka, hapana ndio maana umasikini wetu unazunguka tu,”alisema Kaboyoka.

Mwenyekiti huyo alishauri kuwe na tathmini katika miradi ambayo imekamilika kwa kwenda kwenye eneo la tukio na kuikagua.

Mbunge wa Mlalo, Rashidi Shangazi (CCM) alisema mpango huo ni mzuri na Serikali imetekeleza kwa kiwango kikubwa miradi mikubwa ambayo itaupaisha uongozi wa Rais Dk.John Magufuli.

“Novemba tulitoa maoni yetu na tunashukuru Serikali sikivu imeyachukua hakika ni jambo jema na tunaendelea kujivunia Serikali yetu,”alisema Shangazi.

Naye Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni (CCM) alisema amefurahishwa na kwa jinsi ambavyo Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ambapo alidai inawasaidia kutoa ajira kwa watanzania wengi.

“Sasa tuondoe ukiritimba katika suala la uwekezaji kwa sababu hili ni eneo muhimu sana kwetu na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza uimarishwe pamoja na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe,”alisema Chegeni.

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) alidai kwamba Serikali imechukua miradi mingi mikubwa na inataka kutekeleza kwa wakati mmoja jambo ambalo haliwezekani.

“Huu ni mpango wa muda mrefu na mfupi shida ni katika kipindi hichi Serikali imechukua miradi mingi hivyo fedha zinazotumika ni nyingi wasiwasi wangu kama miradi hii itakamilika kwa wakati,”alisema Kubenea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles