27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mrema awagomea wapinzani wenzake

AZIZA MASOUD – Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, amesema hawezi kuungana na vyama vingine vya upinzani vilivyofungua kesi kupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018.

Amesema anaamini kufanya hivyo hakuwezi kuondoa matatizo yaliyopo ambayo msingi wake unatokana na ubovu wa sheria zilizopo.

Mrema ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja kupita baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuanza kusikiliza kesi namba 31 ya kupinga muswada huo iliyofunguliwa mahakamani hapo Desemba 20 mwaka jana na viongozi wa vyama vya upinzani.

Viongozi hao ni Kiongozi Mkuu ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Kaimu Katibu Mkuu Cuf (Bara), Joram Bashange na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani.

Katika kesi hiyo mshtakiwa mkuu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilangi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwake Salasala, Dar es Salaam, Mrema alisema wapinzani wanapaswa kufahamu kuwa hitaji la sasa la nchi ni marekebisho ya sheria kwa ujumla na si sheria moja moja.

“Siwezi kuungana na wapinzani kumshtaki AG, hii nchi inahitaji marekebisho makubwa ya sheria zinazotumika. Kwa uzoefu wangu wa kisiasa na nyadhifa nilizowahi kushika ikiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, kuna haja ya kufanya marekebisho, hii itasaidia pia kuwalinda viongozi akiwamo Rais,” alisema Mrema.

Alisema anaamini mawazo ya wapinzani wenzake kuupinga muswada huo ni mazuri, lakini jambo hilo litafanikiwa na kuwa na tija kama wanalifanya kwa nia nzuri kwa taifa.

“Wapinzani sisi tunajuana, hofu yangu kuwa ni kweli huu muswada wanaupinga kwa nia nzuri, wapinzani wajiangalie sana, kama kweli wanachokitafuta wanataka kusaidia nchi na kusimamia mageuzi ya maendeleo waendelee, lakini kama wanafanya hivyo huku wakiwaza kupata vyeo haitosaidia,” alisema Mrema.

Akizungumzia kuhusu tuhuma anazopewa na wapinzani wenzie huku wakimwita ni mwanachama wa CCM kutokana na misimamo yake hasa wa kumtetea Rais Dk. John Magufuli, alisisitiza kuwa ataendelea kufanya hivyo kwa sababu ni haki yake.

“Wananiambia mimi ni mwanachama wa CCM, wananiandama kila siku, nawashangaa kwani mimi nina alama gani mpaka wakaniite ni CCM,  kuna kitu gani ambacho nakifanya si sahihi wakati wanajua kabisa mimi ndiye mwasisi wa siasa hizi za upinzani tangu mwaka 1995.

“Wapo wengine wananiambia nimezeeka niache siasa nilee wajukuu, mimi sijazeeka, nataka niwape taarifa ninaishi vizuri na wajukuu zangu, hawana shida yoyote na wao ndio wananiwezesha katika harakati zangu za kufanya siasa,” alisema Mrema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles