30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe, Matiko kuanika ya gerezani


Na MWANDISHI WETU

BAADA ya kutoka gerezani walikokaa kwa zaidi ya miezi mitatu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, wanajipanga kufunguka kwa umma.

MTANZANIA Jumamosi limedokezwa siku na saa yoyote kuanzia sasa Mbowe na Matiko watazungumza kuhusu masuala mbalimbali yanayokigusa chama chao, hali ya siasa na zaidi lile la maisha yao ya siku 104 gerezani, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana kabla ya juzi Jaji wa Mahakama Kuu, Sam Rumanyika, kutengua uamuzi huo.

Taarifa za Mbowe na Matiko kujiandaa zilithibitishwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, ambaye alisema vigogo hao watazungumza hivi karibuni, ingawa hakutaja siku.

Pamoja na jitihada za kuwapata Mbowe ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Hai pamoja na Matiko kugonga mwamba jana, kutokana na simu zao kuita pasipo majibu, vigogo hao wanatazamiwa kuzungumzia namna walivyoishi na waliyoyaona kwa miezi mitatu na siku 11 wakiwa mahabusu.

Si hilo tu, bali vigogo hao, hususan Mbowe, ndiye kiongozi wa Chadema anayetarajiwa kugusia hali ya siasa kwa sasa ndani ya chama chao, hasa wakati huu ambao aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amewakimbia na kurudi CCM, wakati yeye akiwa mahabusu.

Mbowe anatarajiwa kugusia hali ya chama chake ili kutoa ahueni kwa wafuasi wa Chadema ambao wana shauku ya kujua  kinachoendelea.

Itakumbukwa kabla ya Jaji Sam Rumanyika kutamka kuwa Mbowe na Matiko walishinda rufaa hiyo juzi, wabunge hao wawili walifutiwa dhamana Novemba 23, mwaka jana na hivyo walikata rufaa dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, wakipinga kufutiwa dhamana.

Kesi inayowakabili washtakiwa hao pamoja na wenzao ina mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16 mwaka 2018.

Wakati Mbowe na Matiko wakiwa nje kwa dhamana, itakumbukwa

katika kesi inayowakabili ya jinai namba 112 wapo washtakiwa wengine, ambao ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji,

 Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya.

Kuachiwa kwa Mbowe na Matiko kumekuja katika wakati ambao pia wabunge wengine wa chama hicho wakiwa wanasota mahabusu kwa makosa tofauti.

Wabunge hao ni Suzan Kiwanga na Peter Lijualikali pamoja na wanachama saba wa Chadema, ambao nao juzi walishinda dhidi ya ombi la kupinga dhamana lililotolewa na upande wa Jamhuri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro.

Ingawa wabunge hao pamoja na wenzao saba walirudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana juzi, tayari walikuwa wamekaa rumande kwa wiki mbili, wakikabiliwa na makosa ya kufanya vurugu wakati wakipinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Sofi, Novemba 26, 2017.

Mbowe, Matiko, Susan na Lijualikali wanaingia katika orodha ya wabunge wengine wa upinzani wanaokabiliwa na kesi mbalimbali mahakamani.

Wabunge wengine wa upinzani wanaokabiliwa na kesi ni Zitto Kabwe, Tundu Lissu, Selemani Bungara (Bwege), Godbless Lema, Cecil Mwambe, Zubeda Sakuru, Peter Msigwa, Pascal Haonga na Frank Mwakajoka.

Kwa upande wa Lema, ambaye ni Mbunge wa Arusha Mjini, anakabiliwa na kesi ya uchochezi iliyomsababisha kukaa mahabusu kwa siku 121, baada ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuweka zuio la dhamana.

Lema alikamatwa Novemba 2, 2016 na kupata dhamana Machi 3, 2017, baada ya kukaa mahabusu ya Gereza la Kisongo kwa miezi minne akikabiliwa na makosa ya uchochezi.

Mbunge wa Singida Mashariki, Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema anayeendelea na matibabu nchini Ubelgiji, anakabiliwa na kesi zaidi ya tatu za uchochezi.

Mwingine ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini, Msigwa anakabiliwa na kesi kadhaa, ikiwamo iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa.

Mbunge huyo na wenzake wanadaiwa kuchoma moto nyumba ya Mary Tesha, aliyokuwa akiishi Katibu wa Umoja wa CCM (UVCCM), Alphonce Muyinga.

Zitto, ambaye ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge Kigoma Mjini, naye anakabiliwa na kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inayoendelea kusikilizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles