23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii yatakiwa kutambua misingi ya uhuru wa habari

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeitaka jamii kutambua misingi ya uhuru wa habari ili kulinda na kuzuia mashambulizi dhidi ya wanahabari.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga na alisema wanatumia siku ya maadhimisho ya uhuru wa habari kukumbuka mashambulio dhidi ya wanahabari na kuenzi wanahabari walioleta mabadiliko chanya katika tasnia ya habari.

“Kituo kinapenda kukumbusha wadau wa vyombo vya habari kudumisha misingi imara ya vyombo vya habari ili kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari Tanzania,” alisema.

Pia alisema wanatoa wito kwa vyombo vya dola kuhakikisha ulinzi wa uhuru wa kukusanya taarifa na kutoa maoni kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mikataba ya kimataifa ili kudumisha dhana ya uhuru wa kujieleza.

Katika hatua nyingine, LHRC wametambulisha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa na matukio ya haki za binadamu kwa njia ya kidijitali kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo wananchi wa kawaida, waangalizi/watetezi wa haki za binadamu na wadau wengine wa haki za binadamu.

Anna alisema mfumo huo utasaidia kujua changamoto za masuala ya haki za binadamu yanayotokea maeneo mbalimbali na kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwamo Jeshi la Polisi.

Alisema walifikiria kuanzisha mfumo huo baada ya kuona kuwa kuna changamoto kubwa ya utolewaji taarifa wa haki za binadamu hasa kutoka kwa wananchi, walinzi na watetezi wa haki za binadamu.

“Mfumo huu wa kidijitali upo kwa njia za kisasa na rafiki kwa watu wote. Mfumo huu umetengenezwa ili uweze kutumia tovuti, simu janja lakini pia kutumia sms za kawaida. Kwa mantiki hiyo ni wazi utaweza kutumiwa na watu wa aina zote.

“Taarifa ambazo zitakusanywa zitafanyiwa kazi na wafanyakazi wa kituo na kufanya ufuatiliaji kwa Jeshi la Polisi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, mahakama, wizara mbalimbali na taasisi nyingine.

“Ni matumaini yangu kuwa wadau wote, hasa wananchi, wataupokea mfumo huu kwa mikono miwili na kuutumia ipasavyo ili kwa pamoja tuweze kulinda na kutetea haki za binadamu Tanzania,” alisema Anna.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles