23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali ya Mkapa yaanza kupandikiza figo

ARODIA PETER-DODOMA

HOSPITALI ya Rufaa ya Benjamini Mkapa iliyopo mkoani Dodoma, imeweza kupandikiza figo kwa wagonjwa nane kwa mafanikio makubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea hosptali hiyo mwishoni mwa wiki, Daktari Bingwa wa Figo, Kessy Shija, alisema huduma hiyo ya kupandikiza figo ilianza mwaka jana na hadi sasa wagonjwa nane wamekwishapatiwa matibabu hayo.

Mbali na figo, alisema hospitali hiyo inatoa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa moyo kama ilivyo kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.

Akizungumzia ugonjwa huo, Dk. Shija alisema magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu mara nyingi yanasababisha figo kushindwa kufanya kazi.

Kuhusu matibabu, alisema hospitali hiyo inavyo vifaa vya kutosha kwa ajili ya tiba hiyo licha kwamba ni gharama kubwa.

Kutokana na hali hiyo, alitoa wito kwa Watanzania kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa sababu magonjwa ya kudumu kama figo yanachukua gharama kubwa.

“Mathalani matibabu ya figo hukuchua wastani wa kati ya Sh 200,000 hadi 250,000 kwa wiki sawa na Sh milioni mbili kwa mwezi kwa ajili ya kusafishwa, huku tiba ya kupandikiza figo ikichukua wastani wa Sh milioni sita kwa mgonjwa mmoja.

“Hivyo, niwaombe Watanzania kujiunga na NHIF ili wakipata magonjwa ya kudumu kama haya waweze kupata unafuu wa matibabu, kwa sababu wale wasio na bima ya afya wanaoweza kumudu gharama hizo ni wachache sana,” alisema Dk. Shija.

Daktari huyo alisema kujengwa kwa hospitali hiyo mkoani Dodoma kumepunguza rufaa na kwenda nje ya nchi hususan India kufuata tiba hiyo ya upandikizaji figo kwa gharama kubwa.

Kuhusu sababu za ugonjwa huo, daktari huyo alisema zinatokana na mfumo wa maisha.

“Kutokana na mfumo wa maisha uliopo hivi sasa, nchi zinazoendelea ikiwamo  Tanzania wanaougua ugonjwa huo wanaanzia kati ya wastani wa miaka 35 na 44, huku nchi zilizoendelea wanaougua ugonjwa huo huanzia kati ya miaka 60 na kuendelea.

Kazi kubwa ya figo mwilini ni pamoja na kutoa uchafu na maji kwenye mwili, kuzuia shinikizo la damu, kusawazisha kemikali na kuzalisha chembechembe za damu nyekundu mwilini.

Dalili za awali za ugonjwa wa figo ni pamoja na kuvimba miguu, uso pamoja na kutokwa mkojo kidogo tofauti na kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles