30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Chonde chonde bodaboda zinazobeba watoto wadogo

NA AMON MTEGA-SONGEA

BODABODA na bajaji kama vilivyo vyombo vingine vya moto zinaongozwa na sheria kuu mbili.

Sheria ya kwanza ni Sheria ya Usalama Barabarani (The Road Traffic Act, cap. 168) na Sheria ya Utoaji wa Leseni za Usafirishaji (Transport Licensing Act), ambapo chini yake kuna kanuni zinazoitwa kanuni za usafirishaji kwa njia ya bajaji na pikipiki za mwaka 2010.

Kwa kuongezea, bodaboda na bajaji wanafungwa pia na sheria za Serikali za Mitaa (Manispaa, majiji, wilaya).

Kabla na baada ya kuruhusiwa kisheria, pikipiki maarufu bodaboda zimekuwa msaada mkubwa katika mbadala wa usafiri nchi nzima hususani vijijini na katika miji midogo inayoendelea kukua ambapo hakuna magari mengi na kwingine hayapo kabisa.

Usafiri huo umetokea kushika kasi na kuwa maarufu kwa matumizi ya jamii na umesaidia kupunguza gharama za usafiri, rasilimali fedha pamoja na kuokoa muda tofauti na zamani ambapo watu wengi walikuwa wakitembea kwa miguu au baiskeli kwa umbali mrefu, hivyo kupoteza muda na hata wagonjwa kushindwa kufika hospitali kwa wakati.

Hata hivyo, licha ya usafiri huo kupunguza gharama za maisha, baadhi ya wazazi wameanza kuutumia usafiri huo kinyume cha sheria na kanuni na hata kuhatarisha usalama na maisha ya watoto kama tutakavyobainisha katika makala haya.

Katika makala haya, tutajadili namna wazazi pamoja na waendesha bodaboda hizo wanavyokiuka sheria inayozuia mtoto mwenye umri wa chini ya miaka tisa asibebwe kwenye pikipiki peke yake kama abiria.

Mathlani katika Manispaa ya Songea, watoto wanaosoma shule za awali na msingi ambao hawajafikisha umri unaotajwa kisheria, wamekuwa wakitumia usafiri huo kila siku, jambo ambalo linatishia usalama wa watoto hao.

Kimsingi wazazi wameamua kuweka rehani usalama na maisha ya watoto wao kwa madereva wa bodaboda ambao licha ya kuvunja sheria na kanuni ya usafirishaji, baadhi yao wamekuwa wakilalamikiwa kwa uendeshaji mbovu ikiwemo mwendo kasi.

Katika mitaa na viunga vya Manispaa ya Songea, MTANZANIA limebaini kuwapo kwa idadi kubwa ya watoto wa shule za msingi na awali ambao wanatumia usafiri huo huku wengine wakipakizwa wawili hadi wanne kwenye pikipiki moja.

Licha ya sheria kukataza watoto wenye umri mdogo kupandishwa kwenye bodaboda bila kuwapo mtu mzima, sababu nyingine kubwa ni kutokana na watoto kutokumudu ipasavyo kumudu changamoto zinazoweza kujitokeza barabarani zikiwamo dereva kushika breki ghafla, kutovaa kofia ngumu kwa kuwa maumbile ya vichwa vyao bado ni madogo. 

Aidha, wale watoto wanaopakizwa zaidi ya mmoja kwenye pikipiki moja, hawawezi kuvaa kofia hizo wote hata kama zingekuwepo za saizi zao.

Kibaya zaidi baadhi ya waendesha bodaboda wamekuwa wakitumia mipira ya kufungia mizigo na vifurushi kwenye pikipiki kwa kuwafunga watoto hao ili kuwazuia wasiyumbe wawapo barabarani.

Jambo hilo si tu ni hatari kwa watoto bali pia linakiuka haki zao za msingi za watoto zinazolindwa na Katiba ya nchi na sheria za kimataifa.

Kupitia makala haya, tunawasihi  na kuwakumbusha wazazi na walezi kutambua umuhimu wa kuwalinda watoto wao bila kuathiri afya na maisha yao muda wote na kuhakikisha wanakwenda na kurudi shuleni salama.

 Aidha, Serikali kupitia Serikali za mitaa, vijiji na maofisa wa ustawi wa jamii, wasikwepe jukumu lao, wawe na utaratibu wa kuitisha mikutano na jamii kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo jukumu la kuhakikisha usalama wa watoto muda wote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles