24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yaonya Muungano kutochezewa na wanasiasa

Na MWANDISHI WETU-MOROGORO

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wanasiasa wa vyama vya upinzani kutumia kwa weledi na umakini majukwaa ya kisiasa kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Pia kimesema kuwa suala hilo la Muungano ni lazima liangaliwe kwa masilahi mapana kwani limegusa maisha ya watu wa pande zote mbili na katu hakiko tayari kuona unataka kuvurugwa.

Akizungumza jana mjini hapa kuhusu maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano yanayofanyika leo, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, alisema wanasiasa wanaotumia Muungano kama mtaji wa kujitafutia umaarufu waungwe mkono na wananchi sasa hakuna budi kuepukwa kwani wanaweza kuleta madhara kwa jamii na nchi.

Alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar licha ya kuwa na nia njema, udugu na asili, unadumisha mila na jadi za wananchi wake, ukibeba maisha ya watu zaidi ya milioni 55 baada ya miaka 55 kupita tangu ulipoundwa.

“Wanasiasa waache kutumia kasoro ndogondogo zilizopo katika Muungano kusaka kiki za kisiasa. Muungano ni tunu na pia ni jambo nyeti linalobeba maisha na usalama wa watu. Kuna wananchi ambao hawakuona ukoloni ila wanatambua Muungano kwani wamezaliwa wakijikuta huru na wamoja kwa miongo kadhaa sasa,” alisema.

Shaka alishangazwa na wanasiasa wanaotumia dosari za Muungano kwa lengo la kufikia malengo yao kisiasa au matamanio yao ya kupata madaraka kwa kuwataka waache kwani wanaweza kuleta misiba na majuto kutokana na kauli zao.

“Vinywa vya wanasiasa viwe na ashakum ya kuchagua maneno. Visibomoe kuta zinazolinda Muungano, bali zijenge dhamira njema, isiwe njiti za kiberiti karibu na mapipa ya petroli na zisitoe cheche na moto kwani Muungano una maisha ya watu na usalama wao,” alisema.

Alisema ikiwa kuna watu bado wanafikiri Muungano ni wa faida kwa kina marehemu Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Karume au kwa TANU na ASP, huo kwao utakuwa ni mtazamo hasi.

“Muungano umekusanya watu wa makabila tofauti, dini, mila, desturi na maisha yao kwenye mikoa yote. Anayesaka madaraka na asake kivyake ila asichezea Muungano.

“Tubishane, tulumbane na kutaniana kwa mambo mengine bila kudhihaki Muungano,” alisema Shaka

Alisema wanasiasa ndio waliosababishia Muungano wa Libya na Misri kuvunjika mapema pamoja na ule wa Ghana na Guenea, Senegal, Gambia na Mali ambao pia nao ulivurugika.

Shaka aliwataka wanasiasa wa Tanzania na Afrika kujifunza kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani ambayo sasa yamekuwa yakipiga hatua kutokana na faida ya kuungana kwao.

“Uingereza, Ujerumani na Marekani ni mataifa yenye asili ya muungano kihistoria. Wanasiasa wake wanazungumza mengine katika mustakabali wao bila kuhatarisha miungano yao. Marekani hutashuka chini ya jukwaa mtu mmoja ukihamasisha nchi moja ijitoe katika muungano wa nchi zao 52,” alisema.

Hata hivyo katibu huyo amepongeza juhudi za marais Dk. John Magufuli na Dk. Ali Mohamed Shein kwa umakini na umahiri walioonesha katika kulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania katika uongozi wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles